Uchaguzi wa rais Somalia waahirishwa, wabunge wakutana

Bunge jipya nchini Somalia hii leo lilitarajiwa kuchagua rais mpya wa nchi hiyo katika uchaguzi ambao unaelezwa kuwa ni wakihistoria baada ya kumalizika muda wa serikali ya mpito lakini kuna taarifa za kuahirishwa kwa uchaguzi huo ingawa bunge litakuna kwa ajili ya kikao cha kawaida.
Taarifa kutoka ndani ya Bunge hilo ambalo liliteuliwa na viongozi 135 wa wazee wa kimila zimesema kuna kazi ya kufanywa na bunge hilo kabla ya kuchaguliwa kwa rais.
Uchaguzi huo ambao umevuta hisia za watu wengi unatarajiwa kuwa wenye mvutano mkali kati ya rais anayemaliza muda wake Sheikh Sharif Ahmed, waziri mkuu Abdiweli Mohamed Ali na spika wa bunge Sharif Hassan Sheikh Adan ambao wote kwa pamoja wanawania nafasi hiyo.
Uchaguzi huo unafanyika wakati ambapo ripoti iliyotolewa mwezi Julai mwaka huu na Umoja wa Mataifa umeitaja serikali iliyomaliza muda wake kukithiri kwa vitendo vya rushwa jambo ambalo rais Sheikh Sharif alikanusha vikali.
Nchi ya somalia imekosa serikali imara toka mwaka 1991 alipoangushwa rais Mohamed Siad Barre.
Uchaguzi huo ni dalili za Somalia kuanza kurejea katika hali yake ya kawaida baada ya misukosuko ya muda mrefu huku ikikabiliwa na majanga mbalimbali ikiwemo njaa.
Rais atakayechaguliwa atakabiliwa na changamoto kubwa ya kuongoza nchi hiyo ambayo kwa kipindi kirefu imekuwa ikipambana na kundi Al Shabab lenye uhusiano na kundi la Al aeda.
Somalia inafungua ukurasa mpya kuelekea demokrasia baada ya kukosa serikali kwa zaidi ya miaka 20 na Jumuiya ya Kimataifa kupitia Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika wanafanya kila jitihada za kuisaidia Somalia.







MAELEZO
Tuma maoni yako kwa makala haya