Pata taarifa kuu
MISRI

Wanahabari wa Al- Jazeera wahukumiwa jela miaka 7 nchini Misri

Mahakama jijini Cairo nchini Misri, imewahukumu  miaka 7 jela Wanahabari watatu wa Al-Jazeera baada ya kupatikana na kosa la kuripoti habari za uongo na kushirikiana na kundi lililoharamishwa la Muslim Brotherhood.

Wanahabari wa Al Jazeera
Wanahabari wa Al Jazeera
Matangazo ya kibiashara

Hukumu hiyo imetolewa siku ya Jumatatu dhidi ya Wanahabari hao Peter Greste, Mohamed Fahmy na Baher Mohamed ambao wamekuwa wakikanusha tuhma hizo.

Ni hukumu ambayo imewashangaza na kushtumiwa na serikali ya Australia, wanaharakati wa kutetea haki za Binadamu likiwemo la Amnesty International ambalo limekuwa likishikiniza kuachiliwa huru kwa wanahabari hao.

Greste raia wa Australia ambaye makao yake makuu yalikuwa jijini Nairobi nchini Kenya, Fahmy raia wa Misri watakitumikia kifungo cha miaka 7 jela lakini Baher Mohamed yeye atafungwa miaka mitatu zaidi na kwa jumla kuwa miaka 10 baada ya kupatikana na silaha.

Wanahabari wengine wa Al Jazeera Alaa Bayoumi, Anas Abdel-Wahab Khalawi Hasan, Khaleel Aly Khaleel Bahnasy, Mohamed Fawzi, Dominic Kane na Sue Turton na ambao hawakuwa Mahakamani, wamehukumiwa jela miaka 10.

Kituo cha Al Jazeera kimekuwa kikiendelea kushtumu  na kupinga kushtakiwa kwa Wanahabari wao na kusema hawakufanya makosa yoyote.

Wakati wa hukumu hiyo, Greste, Fahmy na Baher walionekana wenye huzuni kubwa baada ya Jaji kusoma hukumu hiyo.

Waziri wa Mambo ya nje wa Australia Julie Bishop, amesema serikali yake imehuzunishwa mno na hukumu hiyo na kumtetea Greste ambaye amesema hakufanya kosa lolote wakati akifanya kazi yake.

“Tutazungumza na rais wa Misri Fatah Al Sisi moja kwa moja kuona kama kuna uwezekano yeye kuingilia kati suala hili,” Julie Bishop ameongeza.

Aidha, Waziri Bishop ameongeza kuwa huu ni wakati mwafaka kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kuishinikiza serikali ya Misri kuwaachilia huru wanahabari hao.

Familia ya Greste inasema kuwa inawasiliana na Mawakili wake, ili kukata rufaa dhidi ya kifungo hicho.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.