Pata taarifa kuu
RWANDA-FDLR-Usalama

Rwanda : FDLR yaomba mazungumzo na Kigali kabla ya wapiganaji wake kuweka silaha chini

Serikali ya Rwanda ambayo inapinga mazungumzo ya kisiasa na kundi la waasi la FDLR, imewataka wapiganaji wa kundi hilo kurejea nchini kwa hiari ili wajumuike na wengine kwa ujenzi wa taifa. Tangu mwaka 2001, wapiganaji wa zamani 11,000 wa FDLR walirejea nchini Rwanda.

Kundi la wapiganaji wa FDLR, nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo (picha ya zamani).
Kundi la wapiganaji wa FDLR, nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo (picha ya zamani). Reuters
Matangazo ya kibiashara

Rwanda ni nchi ambayo imepiga hatua katika sekta ya uchumi, lakini imekua ikinyooshewa kidole kwa ukiukwaji wa haki za binadamu. Kundi hilo la waasi wa Rwanda limetoa masharti ya kuanzishwa kwa mazungumzo na serikali ya Kigali kabla ya wapiganaji wake kurejea nchini.

Msimamo huo wameuweka wazi baada ya mkutano wa viongozi wa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu uliyofanyika Agosti 14 mjini Luanda, nchini Agola, ambao uliwataka waasi hao kuweka silaha chini kabla ya tarehe 31 mwezi Desemba mwaka huu ili kuepuka hatua za kijeshi, hatua ambayo imekaribishwa na mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, Martin Kobler.

“Harakati za kijeshi ziko mbiyoni”, amesema Martin Kobler, huku akitolea wito wapiganaji wa FDLR kurejea nchini kwa hiari. Kwa mujibu wa Kobler, wapiganaji wa zamani 11,000 wa FDLR walirejea nchini Rwanda katika mazingira mazuri.

Wapiganaji wa zamani wa FDLR wanaorejea nchini Rwanda wamekua wakipokelewa katika kambi ya wapiganaji wanaorejeshwa katika maisha ya kiraia ya Mutobo kaskazini mwa Rwanda. Kambi hiyo inafanya kazi tangu mwanzoni mwa mwaka 2000. Katika kambi hiyo wamekua wakipewa mafunzo ya uraia yenye misingi ya uzalendo, ujenzi na maridhiano. Baada ya mafunzo wamekua wakipewa pesa za Rwanda 200,000 sawa na Euro 200 kama ahadi ya kutofuatiliwa na vyombo vya sheria vya Rwanda, iwapo watakuwa hawajahusika katika mauaji ya kimbari yaliyotokea mwaka 1994, ambapo watu zaidi ya 800,000 kutoka jamii ya watutsi na wahutu wenye msimamo wa wastani waliuawa.

Kiongozi wa Tume inayohusika na kuwarejesha wapiganaji wa zamani katika maisha ya kiraia, Jean Sayinzoga, amesema wapiganaji wa zamani wa FDLR waliyokubali kukiri kuhusika katika mauaji ya kimbari walipunguziwa hadi nusu ya adhabu waliyohukumiwa

Kwa upande wake msemaji wa FDLR, La Forge Fils Bazeye, amesema ana hofu na ushawishi huo wa Kigali, na kuomba wahakikishiwe usalama wao.

“Martin Kobler ninamuheshimu, lakini hana taarifa yoyote kuhusu hali inayojiri nchini Rwanda, hususan madhila wanayofanyiwa wanyarwanda ambao wanapinga utawala wa paul Kagame, utawala ambao hauheshimu haki za binadamu”, amesema Bazeye, huku akishuku kwamba huenda Martin Kobler anahusika kwa njia moja ama nyingine katika harakati za kuwarejesha Rwanda kwa lengo la kuwamalizia maisha.

Bazeye amesema wapiganaji wa FDLR wako tayari kurejea nchini Rwanda, lakini hawatakubali kurejeshwa kiholela kama kondoo wanaobebwa machinjoni.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.