Pata taarifa kuu
TANZANIA-CUF-VURUGU-USALAMA-SHERIA-SIASA

Wafuasi wa chama cha CUF wasalia rumande

Wafuasi takribani 32 wa chama cha upinzani nchini Tanzania cha CUF, wamerejeshwa rumande kutokana na kukosekana kwa dhamana, kwa mujibu wa Mahakama ya Kisutu.

Anna Makinda, Spika wa Bunge la Tanzania.
Anna Makinda, Spika wa Bunge la Tanzania. RFI-KISWAHILI
Matangazo ya kibiashara

Wafuasi hao wamefikishwa mahakamani Alhamisi wiki hii, baada ya kukamatwa na polisi kufuatia maandamano ambayo polisi imesema yamekua yamepigwa marufuku.

Wakati huo huo Bunge la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania leo Alhamisi limejadili kitendo cha “uvunjifu wa amani”, kwa mujibu wa polisi, kiliotokea katika maandamano ya CUF yaliyoongozwa na kiongozi wa chama hicho, Profesa Ibrahimu Lipumba jijini Dar es Salaam.

Katika mjadala huo Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe aliomba suala hilo kupewa muda wa kuchunguzwa kwa kina na vyombo husika.

Hata hivyo Mwanasheria mkuu, George Masaju, ametaka suala hilo lisijadiliwe bungeni kwa kile alichosema Mahakama imeanza kulishughulikia.

George Masaju amesema kujadili suala hilo bungeni ni kukiuka sheria ya mgawanyo wa madaraka katika mihimili ya dola, jambo ambalo lilipingwa na idadi kubwa ya wabunge.

Waziri Chikawe katika taarifa yake ameeleza kuwa taarifa za uchunguzi wa ndani zilipelekea jeshi la Polisi kuwaomba Cuf kutofanya maandamano yao kwa kuhofiya kudorora kwa usalama.

Kwa upande wake Spika wa Bunge, Anna Makinda, alitoa muda wa dakika 10 kwa wabunge kujadili suala hilo huku mbunge Tundu Lissu akilaani vikali kutokea kwa vurugu hizo na akitaka kuwajibika kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Mwanasheria mkuu pamoja na waziri Chikawe kwa kuwa vitendo vinavyoendelea vinashabihiana na kauli yake ya “wapigwe tu”.

Aidha wabunge wengi wa kambi ya upinzani wakichangia hoja hiyo kwa jazba walionyesha kukerwa na kuzilaani vurugu hizo, huku wabunge wa CCM wakitaka kusimamiwa kwa sheria bila kupendelea mtu yeyote.

Spika Makinda alihitimisha kwa kusema kuwa anaiomba serikali kufanya uchunguzi kupitia vyombo vyake.

Hayo yakijiri CUF imeapa kuendelea na maandamano kila mwaka.

Katika maadhimisho yaliyofanyika mwaka huu, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na wanachama 32 wa chama hicho walipigwa kisha kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa madai ya kuendesha maandamano yasiyokuwa na kibali.

Chama cha Wananchi (CUF) kimesema, hakitarudi nyuma na kitaendelea kufanya maandamano na mikutano ya hadhara kila Januari 26 na 27 kila mwaka kuazimisha mauaji ya wanachama wake yaliyotokea Zanzibar mwaka 2001.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.