Pata taarifa kuu
BURUNDI-SIASA

Baadhi ya vigogo katika chama cha Cndd-Fdd wafukuzwa katika chama

Mpasuko umeendelea kukikumba chama tawala nchini Burundi cha Cndd-Fdd. Orodha ya vigogo ambao ni wafuasi wenye ushawishi mkubwa katika chama hicho wanaopinga rais Pierre Nkurunziza kugombea muhula wa tatu imeendelea kuongezeka.

Festus Ntanyungu, mbunge na waziri wa zamani, akiwa msemaji wa kundi la vigogo katika chama tawala Burundi cha Cndd-Fdd wanaopinga Rais Pierre Nkuruziza kugombea muhula wa tatu.
Festus Ntanyungu, mbunge na waziri wa zamani, akiwa msemaji wa kundi la vigogo katika chama tawala Burundi cha Cndd-Fdd wanaopinga Rais Pierre Nkuruziza kugombea muhula wa tatu. Esdras Ndikumana / RFI
Matangazo ya kibiashara

Mbali na idadi ya watu kumi na saba waliotia saini hivi karibuni kwenye waraka wa kumtaka rais Nkurunziza kutogombea muhula wa tatu, wafuasi wengine 79 wenye ushawishi mkubwa katika chama cha Cndd-Fdd wameungana na wengine kumi na saba kwa kutia saini kwenye waraka huo.

Hata hivyo vigogo kumi kati ya kumi na saba ambao walitia saini kwa mara ya kwanza kwenye waraka huo wamefutwa katika chama hicho. Uamzi huu umechukuliwa Jumatano wiki hii, kwa mujibu wa msemaji mpya wa chama cha Cndd-Fdd, Gélase Daniel Ndabirabe.

Uongozi wa chama cha Cndd-Fdd unawachukulia vigogo hao kama waanzilishi wa vuguvugu linalomtaka rais Pierre Nkurunziza kutogombea muhula wa tatu.

Wafuasi hao wenye ushawishi mkubwa waliofukuzwa katika chama cha Cndd-Fdd ni pamoja na msemaji wa rais Léonidas Hatungimana (mzaliwa wa mkoa wa Cankuzo), aliye kuwa msemaji wa chama cha Cndd-Fdd Onésime Nduwimana (mzaliwa wa mkoa wa Gitega), mbunge Geneviève Kanyange (mzaliwa wa mkoa wa Kayanza), François Barahemena (mzaliwa wa mkoa wa Bujumbura), Jean Berchimans Niragira (mzaliwa wa mkoa wa Cankuzo), Jean Berchimans Simbakwira (mzaliwa wa mkoa wa Cankuzo), mkuu wa zamani wa mkoa wa Ruyigi Moise Bucumi (mzaliwa wa mkoa wa Ruyigi), Evariste Nsabiyumva (mzaliwa wa mkoa wa Karusi), mkuu wa mkoa wa Bubanza Anselme Nyandwi (mzaliwa wa mkoa Bubanza) pamoja na mkuu wa zamani wa mkoa wa Muramvya Oscar Ndayiziga (mzaliwa wa mkoa wa Muramvya).

Katika mkutano na vyombo vya habari Jumanne wiki hii, kiongozi wa chama cha Cndd-Fdd, Pascal Nyabenda alitangaza kwamba Wabunge, Maseneta na maafisa waandamizi katika serikali waliotia saini kwenye waraka wa kumtaka rais Nkurunziza kutogombea muhula wa tatu watachukuliwa hatua kali hadi kufukuzwa katika chama na kupoteza nafasi zao za katika nyadhifa mbalimbali.

Wadadisi wanasema chama cha Cndd-Fdd kinakabiliwa wakati huu na malumbano ya ndani ya chama na kupelekea chama hicho kugawayika katika makundi matatu : kundi linalomuunga mkono rais Nkurunziza kugombea muhula wa tatu, kundi linalopinga rais  huyo kugombea muhula wa tatu na kundi ambalo halijaonesha msimamo wake, ambalo wengi wanadhani kwamba linaungana na kundi linalopinga rais Nkurunziza kugombea muhula wa tatu.

Idadi ya wanao muunga mkono kwa sasa rais nkurunziza inaoneka kuwa ni ndogo kadri muda unavyokwenda.

Hata hivyo Wabunge, Maseneta, Wakuu wa mikoa na wilaya pamoja na maafisa waandamizi katika taasisi mbalimbali za nchi, ambao wametia saini kwenye waraka huo wamebaini kwamba wameanza kufanyiwa vitisho, lakini wameapa kuendelea na harakati zao.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.