Pata taarifa kuu
MAREKANI-BURUNDI

Marekani yasema Burundi inarudi nyuma kidemokrasia

Marekani imelaani hatua ya rais wa Burundi Piere Nkurunziza kutangaza kuwania urais kwa muhula wa tatu wakati wa uchaguzi Mkuu mwezi Juni mwaka huu.

Rais Pierre Nkurunziza akiwahutubia wafuasi wake wakati wa mkutano mkuu wa CNDD FDD
Rais Pierre Nkurunziza akiwahutubia wafuasi wake wakati wa mkutano mkuu wa CNDD FDD REUTERS/Thomas Mukoya
Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa Mambo ya nje wa Marekani Marie Harf amesema hatua ya chama tawala CNDD FDD kumwidhinisha rais Nkurunziza ni ishara kuwa Burundi inapoteza nafasi ya kuimarisha demokrasia yake.

Marekani imewaomba wananchi wa Burundi kusalia watulivu na kuwataka wanasiasa kuhakikisha kuwa uchaguzi Mkuu unakuwa huru na haki na kusisitiza kuwa inafuatilia kwa karibu hali ya kisiasa nchini humo.

Siku ya Jumamosi Mwenyekiti wa chama tawala Pascal Nyabenda alisema,
“Tungependa kulitangazia taifa na Jumuiya ya Kimataifa kuwa mwanachama aliyeteuliwa kutuwakilisha katika Uchaguzi Mkuu ni rais Pierre Nkurunziza,”.

Nyabenda aliongeza kuwa,” Nkurunziza ana haki ya kuchaguliwa kwa muhula wa tatu,”.

Upinzani na Mashirika ya kiraia yamesema yataanza maandamano leo Jumapili jijini Bujumbura kulaani hatua ya rais Nkurunziza ambayo wanasema ni kinyume cha Katiba ya nchi hiyo inayomtaka rais kuwa madarakani kwa mihula miwil tu kama ilivyokubaliwa katika mkataba wa amani wa Arusha.

Mwanaharakati Pierre Claver Mbonimpa amesema, “ Hatua hii haikubaliki, inakeuka katiba ya nchi,”.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa zaidi ya watu elfu nane tayari wamekimbilia nchini Rwanda kwa hofu ya kuzuka kwa machafuko ya kisiasa nchini humo.

Kuna hofu kuwa, machafuko yaliyoshuhudiwa kati ya mwaka 1993 hadi 2006  yakarejea tena baada ya rais Nkurunziza kutangaza kuwania urais kwa muhula mwingine.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.