Pata taarifa kuu
BURUNDI-VURUGU-EAC

Viongozi waliojaribu kuipindua Serikali ya Burundi wakamatwa, rais Pierre Nkurunziza kulihutubia taifa punde

Jeshi nchini Burundi limekanusha kukamatwa kwa kiongozi aliyehusika na jaribio la kutaka kuipindua Serikali ya rais Pierre Nkurunziza, licha ya kukiri kushikiliwa kwa baadhi ya wanajeshi waliohusika kwenye jaribio hili.

Jenerali, Godefroid Niyombare mwenye miwani ambaye jaribio lake la mapinduzi limeshindikana na kukamatwa
Jenerali, Godefroid Niyombare mwenye miwani ambaye jaribio lake la mapinduzi limeshindikana na kukamatwa EUTERS/Jean Pierre Aime Harerimana
Matangazo ya kibiashara

Polisi nchiniu Burundi inasema kuwa wanajeshi kadhaa waliohusika kwenye jaribio hilo wamekamatwa sambamba na wanajeshi wengine wajuu waliokuwa wanashirikiana na Jenerali Niyombare ambaye mpaka sasa haijaweza kuthibitishwa iwapo amekamatwa.

Mapema usiku wa kuamkia leo, Jenerali Nyombare alitangaza kushindwa kutekeleza mapinduzi aliyoyapanga na kwamba atajisalimisha yeye pamoja na wanajeshi wengine waliokuwa wanamsaidia.

Hatua hii imekuja baada ya wanajeshi walioasi kuzidiwa uwezo na wanajeshi watiifu kwa Serikali ya rais Nkurunziza, ambapo toka juzi walikuwa wanawania kuchukua kituo cha taifa cha Televisheni na Redio.

Jaribio hili la aina yake, limemalizika ndani ya saa 48 baada ya hapo awali kuwepo taarifa kuwa haijulikani ni nani hasa ambaye alikuwa anaumiliki wa Serikali baada ya kushuhudia maandamano ya wananchi wanaopinga rais Nkurunziza kuwania muhula watatu wa urais.

Jenerali Niyombare kwenye mahojiano maalumu ya njia ya simu, amesema kuwa "Tumeamua kujisalimisha, na nimatumaini yetu kuwa hawatatuua".

Kiongozi mmoja wa juu wa Polisi nchini Burundi, amethibitisha kujisalimisha kwa wanajeshi hao, ambapo ameongeza kuwa jenerali Niyombare pamoja na wanajeshi wengine wanaomuunga mkono wamekimbia na wanatafutwa.

Msemaji wa jenerali Niyombare, Zenon Ndabaneze akizungumza na shirika la habari la AFP amethibitisha wanajeshi wao kujisalimisha baada ya yeye mwenyewe kukamatwa na wanajeshi wa Serikali, ambapo pia naibu wake Niyombare, Cyrille Ndayirukiye na wenzake wengine pia wamekamatwa.

"Tumeamua kujisalimisha, tumeweka chini silaha zetu, tumewapigia simu wizara ya mambo ya ndani kuwataarifu kuwa hatuna silaha tena". Alisema Ndabaneze saa chache kabla ya kukamatwa kwake.

Mwandishi wa rfi idhaa ya kiingereza, Danniel Finnan aliyeko mjini Bujumbura, Burundi, amesema kuwa hali kwa sasa imerejea kwenye hali yake ya kawaida licha ya maandamano ya hapa na pale katika baadhi ya maeneo, ambako pia kumesikika milio ya risasi.

Katika hatua nyingine, msemaji wa rais Nkurunziza, amethibitisha kuwa kiongozi wake amerejea mjini Bujumbura usiku wa kuamkia leo na kwamba leo Ijumaa anatarajiwa kulihutubia taifa kupitia njia ya televisheni.

Wakati jaribio hili linafanyika, rais Nkurunziza alikuwa nchini Tanzania, ambako alienda kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na kati, lakini akashindwa kushiriki baada ya kupokea taarifa za jaribio la mapinduzi.

Taarifa zaidi kutoka jijini Bujumbura zinasema kuwa mashirika ya kiraia yametoa wito kwa wananchi kujitokeza tena barabarani kushiriki kwenye maandamano zaidi ya kupinga rais Nkurunziza kuwania urais kwa muhula wa tatu.

Machafuko yaliyoshuhudiwa nchini Burundi kwa takribani majuma matatu sasa, yametokana na hatua ya rais Nkurunziza kutangaza kuwania urais kwa muhula wa tatu licha ya shinikizo la kimataifa kumtaka asigombee.

Juma hili wakati wa mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini dar ee Salaam, Tanzania, walilaani mapinduzi yaliyofanyika nchini Burundi, na kutaka uchaguzi mkuu usogezwe mbele na pia kuheshimiwa kwa mkataba wa Arusha unaotaka rais wa Burundi kuwania urais kwa mihula miwili pekee.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.