Pata taarifa kuu
BURUNDI-UN-AU-ICGLR-EAC-USALAMA-SIASA

Burundi : serikali na chama tawala vyasusia mazungumzo

Chama cha rais wa Burundi Pierre Nkurunziza, cha Cndd-Fdd kimesusia mazungumzo yaliyotishwa tangu Jumanne wiki hii na timu ya usuluhishi ya kimataifa kuhusu mzozo unaoendelea nchini Burundi.

Rais Pierre Nkurunziza, mgombea katika uchaguzi wa urais kwa tiketi ya chama cha Cndd-Fdd.
Rais Pierre Nkurunziza, mgombea katika uchaguzi wa urais kwa tiketi ya chama cha Cndd-Fdd. REUTERS/Thomas Mukoya
Matangazo ya kibiashara

Jumatatu wiki hii timu ya usuluhishi iliwatolea wito wadau wote katika mgogoro wa Burundi kushiriki mazungumzo kwa minajili ya kutafutia suluhu mgogoro huo. Lakini Chama tawala cha Cndd-Fdd na serikali vimesusia kikao cha kwanza cha mazungumzo hayo.

Chama hicho cha rais Pierre Nkurunziza kimetangaza kuwa hakitashiriki kutokana na kampeni ya uchaguzi wa wabunge na madiwani ambayo kinaendesha wakati huu zikisalia siku zisiozidi sita ili ufanyike uchaguzi wa wabunge na madiwani.

Hata chama cha Uprona kinachotambuliwa na utawala wa Pierre Nkurunziza hakikushiriki mazungumzo hayo.

Kwa mujibu wa katibu mkuu wa chama cha Uprona, Gaston Sindimwo, huu siwakati wa mazungumzo. " Mazungumzo yanakaribishwa baada ya uchaguzi, hapana wakati huu", amesema gaston Sindimwo.

Itafahamika kwamba chama cha Cndd-Fdd kimekua kikifutilia mbali uwezekano wowote wa kuandaa kwa makubaliano ya wadau wote katika mchakato wa uchaguzi kalenda ya uchaguzi, pamoja na kuanzisha mazungumzo yatakayowashirikisha wadau wote.

Timu ya usulihishi wa kimataifa ilikutana Jumatatu wiki hii kwa mara ya kwanza mjini Bujumbura. Timu hii inaundwa na Ibrahima Fall kutoka Umoja wa Afrika, Abdoulaye Bathily kutoka Umoja wa Mataifa, Katibu mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Richard Sezibera pamoja na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR ).

Hayo yakijiri hali ya usalama imeendelea kudorora katika maeneo mbalimbali nchini Burundi, hususan katika mji mkuu wa Bujumbura.

Watu zaidi ya wanne waliuawa na wengine zaidi ya ishirini walijeruhiwa katika mashambulizi ya guruneti dhidi ya baadhi ya baa za mikoa ya Kirundo, Ngozi na Kayanza, Kaskazini mwa Burundi.

Mashambulizi haya yalitiokea usiku wa Jumapili kuamkia Jumatatu Juni 22.

Mashambulio haya yalitokea siku moja baada ya mashambulizi mengine yaliyoendeshwa usiku wa Ijumaa kuamkia Jumamosi juni 20 katika wilaya mbalimbali za mji wa Bujumbura. Mashambulizi ambayo yalilenga vituo vya askari polisi.

Askari polisi zaidi ya kumi na mmoja walijeruhiwa katika mashambulizi hayo. Hata hivyo polisi iliwatuhumu waandamanji kuhusika na mashambulizi hayo, tuhuma ambazo waandamanaji walitupilia mbali.

Hali ya hofu imeendelea kutanda katika mji wa Bujumbura, huku kila upande ukiutuhumu mwengine kuhusika na mdororo wa usalama unaoshuhudiwa wakati huu nchini Burundi.

Hayo yakijiri raia wameendelea kuitoroka nchi. Mwishoni mwa juma hili lililopita mamia ya watu walivuka mpaka na kukimbilia nchi jirani za Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Tanzania, kwa mujibu wa vyanzo vya Idara ya uhamiaji nchini Burundi, PAFE.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.