Pata taarifa kuu
RWANDA-UINGEREZA-UHISPANIA-SHERIA

Mkuu wa Idara ya ujasusi ya Rwanda akamatwa London

Emmnuel Karenzi Karake, mkuu wa Idara ya ujasusi wa Rwanda, amekamatwa mjini London na polisi ya Uingereza kufuatia hati ya kukamatwaya Umoja wa Ulaya iliyotolewa na Uhispania.

Mkuu wa Idara ya ujasusi wa Rwanda, Emmnuel Karenzi Karake.
Mkuu wa Idara ya ujasusi wa Rwanda, Emmnuel Karenzi Karake. AFP PHOTO/MONUC
Matangazo ya kibiashara

Emmnuel Karenzi Karake alishtakiwa mwaka 2008 kuhusiana na uchunguzi wa makosa ya jinai kwa ajili ya mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya ubinadamu. Karenzi Karake anatuhumiwa makosa mbalimbali ya uhalifu aliyoyafanya nchini Rwanda na nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wakati na baada ya mwaka 1994, ikiwa ni pamoja na mauaji ya raia wawili wa Uhispania waliokua wakihudumu katika shirika moja la kiutu.

Kukamatwa kwa Emmanuel Karenzi Karake kunakuja miaka saba baada ya kutolewa kwa hati za kimataifa za kukamatwa kwake ziliyotolewa na jaji wa Uhispania, na miaka kumi baada ya kuanza kwa uchunguzi nchini Uhispania, uchunguzi uliyomlenga mkuu huyo wa Idara ya ujasusi ya Rwanda.

Wizara ya mambo ya nje imeithibitisha RFI mapema Jumatatu jioni wiki hii kwamba Karake alikamatwa Jumamosi na polisi wa Metropolitan, bila kutoa maelezo zaidi.

Hata hivyo Uingereza na Rwanda zimekua na uhusiano mzuri na zimekua zikigawana maslahi mengi.

Kwa mujibu wa wakili wa upande wa mashtaka nchini Uhispania, Polisi ya Interpol nchini Uingereza imekutana na polisi ya Interpol ya Uhispania ili kuhakikisha kuwa hati za kimataifa za kukamatwa bado ni halali, ndivyo alivyowathibitisia jaji wa Uhispania.
Tuhuma.

Wakili Jordi Palou Loverdos ana imani kwamba sasa London itakubali kumsafirisha Emmanuel Karenzi Karake ili ahukumiwe nchini Uhispania.

" Emmanuel Karenzi Karake alikuwa mkuu wa ujasusi katika jeshi mwaka 1994 na 1997, sanjari na mauaji mengi nchini wakati wa mauaji ya kimbari, lakini hasa baada ya mauaji hayo, siyo tu nchini Rwanda lakini pia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Na si tu dhidi ya raia wa (Uhispania, Rwanda, na Congo na raia kutoka jamii ya Wahutu), lakini pia uporaji wa mali mashariki mwa Congo, uporaji ambao kwa namna moja au nyingine alifadhili vita ", amesema Jordi Palou Loverdos.

Kigali imeiomba Uingereza kujieleza kuhusu kukamatwa kwa Emmanuel Karenzi Karake. Kwa mujibu wa waziri wa sheria wa Rwanda, Johnson Busingye, mkuu wa Idara ya ujasusi wa Rwanda, alifikishwa mahakamani Jumapli mwishoni mwa juma lililopita na anatazamiwa kufikishwa kwa mara nyingine mahakamani Alhamisi wiki hii.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.