Pata taarifa kuu
BURUNDI-UN-UCHAGUZI

Waangalizi wa UN wadai uchaguzi wa Burundi haukuwa huru na haki

Waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Mataifa wamesema kuwa uchaguzi mkuu wa wabunge na ule wa Serikali za mitaa uliofanyika mwanzoni  mwa juma hili nchini Burundi, haukuwa huru na haki. 

Waandamanaji kwenye wilaya Cibitoke wakiandamana kupinga muhula wa tatu wa rais Nkurunziza
Waandamanaji kwenye wilaya Cibitoke wakiandamana kupinga muhula wa tatu wa rais Nkurunziza AFP PHOTO/ CARL DE SOUZA
Matangazo ya kibiashara

Tangazo hili la waangalizi wa Umoja wa Mataifa linatolewa ikiwa ni siku moja tu imepita toka watu 6 wauawe kwenye machafuko yaliyoshuhudiwa jijini Bujumbura kati ya polisi na waandamanaji.

Uchaguzi wa wabunge na ule wa Serikali za mitaa ulifanyika Jumatatu ya wiki licha ya wito uliotolewa na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon kutaka uchaguzi huo uahirishwe kwa sababu za kiusalama.

Kwenye taarifa iliyotolewa na waangalizi hao, imesema kuwa uchaguzi wa Burundi ulifanyika kwenye mazingira tete ya kisiasa na kwa kuenea kwa hofu na vitisho katika sehemu nyingi za nchi.

Ripoti hiyo yenye kurasa tisa, imeongeza kuwa matukio ya machafuko na kufuatiwa na milipuko ya mabomu kwenye maeneo kadhaa ya nchi wakati wa zoezi la upigaji kura ni wazi hayakuruhusu wananchi kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi huo.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa uliokuwepo nchini humo umehitimisha ripoti yake kwa kudai kuwa mazingira hayakuwa rafiki kwa kufanyika kwa uchaguzi ulio huru, haki na shirikishi.

Matokeo ya uchaguzi wa wabunge bado hayajatangazwa mpaka sasa, huku nchi ya Ubelgiji ikisema kuwa haitatambua matokeo ya uchaguzi huo huku Marekani ikiongeza shinikizo la kimataifa kutaka uchaguzi wa rais wa July 15 mwaka huu uahirishwe.

Machafuko katika jiji la Bujumbura siku ya Jumatano yalisababisha vifo vya watu 6 kwenye ngome ya upinzani ya Cibitoke, mji ambao umeshuhudia maandamano ya kupinga muhula wa tatu wa rais Pierre Nkurunziza.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.