Pata taarifa kuu
KENYA-MGOMO-ELIMU

Mgomo wa waalimu washika kasi Kenya

Wakati mgomo wa waalimu nchini Kenya ukishika kasi, tume ya kuajiri waalimu nchini humo, TSC imetishia kuwa itawakata waalimu hao mshahara wa siku ambazo hawatakuwa wameingia kazini, tangazo ambalo hata hivyo limepuuzwa na waalimu.

Nairobi, mji mkuu wa Kenya, ambako pia kunaripotiwa mgomo wa waalimu
Nairobi, mji mkuu wa Kenya, ambako pia kunaripotiwa mgomo wa waalimu AFP PHOTO / SIMON MAINA
Matangazo ya kibiashara

Katika kile kinachoonekana ni kuendelea kutunishiana misuli kati ya chama cha waalimu nchini Kenya KNUT na tume ya Kuajiri walimu nchini humo TSC, bado inavyoonekana kuwa suluhu ya kumalizika kwa mgomo wa waalumu nchini Kenya itachukua kitambo kupatikana.

Baada ya tangazo la kuanza kwa mgomo juma hili lililotolewa na katibu mkuu wa KNUT, Wilson Sossion, mwenyekiti wa tume ya kuajiri walimu, Lydia Nzomo ameibuka na kuwataka walimu kurejea kazini ama sivyo wakabiliwe na hatua za kinidhamu pamoja na kukatwa mshahara.

TSC kupitia mwenyekiti wake Lydia Nzomo imesisitiza kuwa kwa sasa haina fedha za kuwalipa waalimu hao licha ya uamuzi wa mahakama kuu wa juma lililopita kuitaka Serikali na tume hiyo kuwalipa waalimu nyongeza ya mshahara wa kati ya asilimia 50 na 60.

Katika hatua nyingine maeneo mengi ya nchi yameshuhudia shule za umma zikiendelea kufungwa huku baadhi ya walimu wakiandamana barabarani kupinga hatua ya tume ya kuajiri walimu, huku wanasiasa nao wakitaka Serikali kushughulikia mgomo huo.

Mgomo wa walimu nchini Kenya umeingia siku ya tano hii leo Ijumaa ambapo waalimu wamesisitiza kutorejea kazini wakati huu wanafunzi wa shule za upili na sekondari wakijiandaa na mitihani ya kitaifa bila ya kuwa na waalimu wao.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.