Pata taarifa kuu
BRAZIL-Uchaguzi-Siasa

Brazil: Dilma Rousseff achaguliwa kwa muhula wa pili

Duru ya pili ya uchaguzi imefanyika Jumapili Oktoba 26 nchini Brazil. Kwa jumla ya asilimia 98 ya kura zilizohesabiwa, zinampa ushindi rais anaye maliza muda wake Dilma Rousseff.

Dilma Rousseff katika mji mkuu wa Brazil, Oktoba 26 mwaka 2014 akiwa pamoja na aliye kuwa rais wa Brazil Lula da Silva (katikati).
Dilma Rousseff katika mji mkuu wa Brazil, Oktoba 26 mwaka 2014 akiwa pamoja na aliye kuwa rais wa Brazil Lula da Silva (katikati). REUTERS/Ueslei Marcelino
Matangazo ya kibiashara

Dilma Rousseff amepata asilimia 51.6 za kura dhidi ya mpinzani wake, seneta Aecio Neves ambaye amepata asilimia 48.4 . Raia milioni 142.8 ndio wamepiga kura kumchagua rais mpya wa taifa la Brazil.

Dilma Rousseff ni mwanamke wa kwanza katika historia ya Brazil kuliongoza taifa hilo kwa mihula miwili. Ni ushindi wa kihistoria kwa chama cha kisoshalisti na chama cha wafanyakazi ambavyo viko madarakani kwa kipindi cha miaka 12 sasa. Dilma Rousseff aliungwa mkono katika kampeni zake za duru ya pili ya uchaguzi na rais wa zamani wa Brazil, Lula da Silva, ambaye ni maarufu nchini humo. Dilma Rousseff, mwenye umri wa miaka 66 amechaguliwa kwa kura milioni 3 zaidi ya mpinzani wake kwa jumla ya raia milioni 143 waliojiandikisha kupiga kura.

Muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi, Dilma Rousseff amesambaza ujumbe kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter kwa kuwashukuru wananchi wa Brazil kwa kuweza kumchagua kuiongoza Brazil kwa muhula wa pili wa kipindi cha miaka minne ijayo.

“ Ninawaomba wananchi wa Brazil tushikamane kwa ujenzi wa taifa. Sidhani kwamba uchaguzi huu utasababisha taifa letu kugawanyika mara mbili”, amesema Dilma Rousseff.

Aecio Neves amempongeza mpinzani wake Dilma Rousseff , baada ya kukubali kuwa ameshindwa katika duru ya pili ya uchaguzi huo wa rais, na kumuomba rais huyo mtarajiwa kukomesha kashfa ya rushwa ambayo imekithiri nchini Brazil.

Katika duru ya kwanza ya uchaguzi uliyofanyika mwanzoni mwa mwezi Oktoba hakuna mshindi aliye patikana kati ya watu watatu waliokua wakigombea kwenye kiti cha rais.

Katika hotuba yake baada ya kutangazwa mshindi, Dilma Roussef amesema atawajibika vilivyo katika kipindi cha miaka minne ijayo hasa kukabiliana na mdorodoro wa fedha na kuhakikisha kuwa mali ya umma inatumiwa vilivyo katika malengo yake.

Dilma Rousseff amebaini pia kwamba atashirikiana na wapinzani wake kwa ujenzi wa taifa la Brazil ambalo linahitaji mchango wa wananchi wake kutoka tabaka mbalimbali kwa kuweza kujiendeleza, amesema Dilma Rousseff.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.