Pata taarifa kuu
PAPUA NEW GUINEA

Wanajeshi Nchini Papua New Guinea wafanya mapinduzi kushinikiza uamuzi wa Mahakama uheshimiwe

Wanajeshi nchini Papua New Guinea wamefanya mapinduzi ambayo yameenda sambamba na kumweka chini ya ulinzi wa nyumbani Mkuu wa Majeshi Brigedia Jenerali Francis Agwi wakitaka Waziri Mkuu wa zamani Michael Somare arejeshwe madarakani.

Matangazo ya kibiashara

Wanajeshi hao wamefanikiwa kumuweka chini ya ulinzi Mkuu wa Majeshi pamoja na Makao Makuu ya Jeshi yaliyopo katika Jiji la Port Moresby wakitaka uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa mwezi uliopita utekelezwe.

Jeshi nchini Papua New Guinea linaamini Somare ndiye mwenye uwezo wa kukabiliana na hali ya kisiasa ambayo inashuhudiwa kwa sasa nchini humo kwa kutekeleza matakwa ya kikatiba ya nchi hiyo.

Wanajeshi hao wamemtaka Kanali Mstaafu Yaura Sasa kushika nafasi ya Ukuu wa Majeshi kwa sasa wakati huu wakiendelea kushinikiza madai yao yatekelezwe na serikali chini ya Waziri Mkuu Peter O'Neill.

Kanali Mstaafu Sasa amenukuliwa akisema kuwa wanajeshi hawajafanya mapinduzi bali wanachotaka wao ni kurejeshwa kwenye cheo chake Waziri Mkuu Somare na O'Neill aondoke kwenye wadhifa huo.

Kanali huyo Mstaafu amefanya kikao na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Jeshi na kujitangaza kuwa Kiongozi wa harakati ambazo zinafanywa na wanajeshi ambao wanataka katiba na sheria ya nchi hiyo viheshimiwe.

Kanali Mstaafu Sasa ameagiza mara moja kwa Rais wa nchi hiyo kutekeleza uamuzi wa Mahakama Kuu wa kumrejesha Somare kwenye wadhifa wake wa Uwaziri Mkuu huku akimtaka O'Neill kuitisha kikao cha bunge kutangaza hilo.

Jeshi nchini Papua New Guinea limetoa siku saba pekee kwa serikali chini ya Waziri Mkuu O'Neill kutekeleza madai yao kinyume na hapo huenda wakakamilisha mapinduzi na kuiondoa serikali.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Mkuu Belden Namah amesema wameshafanikiwa kuwakamata maofisa 15 kati ya 30 wa jeshi ambao wamehusika kwenye tukio hilo na wanamtaka Kanali Mstaafu Sasa ajisalimishe mwenyewe.

Hakuna taarifa zinazoeleza ni kwa nini wanajeshi hao wameamua kumpindua Mkuu wa Majeshi na kumvika jukumu hilo Kanali Mstaafu Yaura Sasa kuweza kuongoza wakati huu wakitaka madai yao yafanyiwe kazi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.