Marekani-Somalia - 
Makala iliyochapishwa tarehe : Ijumaa 08 juni 2012 - Taarifa za ivi karibuni : Ijumaa 08 juni 2012

Marekani yatoa Dola Milioni 33 kwa yeyote atakayetoa maelezo kuhusu viongozi wa Al-Shabab

Viongozi wa wanagambo wa Al-Shabab

Na Victor Melkizedeck Abuso

Marekani imetoa Dola Milioni 33 kama zawadi kwa yeyote atakayetoa habari muhimu kuhusu viongozi wakuu wa wanagambo wa kigaidi wa Al-Shabab nchini Somalia.

Kwa mara ya kwanza Marekani imeorodhesha majina ya viongozi wa Al-Shabab inayowatafuta zaidi akiwemo mwanzilishi wa kundi hilo Ahmed Abdi aw-Mohamed.

Dola Milioni 7 zimetengwa kwa yeyote atakayetoa maelezo alikojificha Aw Mohamed ambaye sasa anatafutwa na Marekani kwa kutishia usalama wa Washington DC na mataifa mengine duniani hasa ya Afrika Mashariki na Kati.

Viongozi wengine wa Al-Shabab wanaotafutwa ni pamoja na Ibrahim Haji Jama, Fuad Mohamed Khalaf, Bashir Mohamed Mahamoud na Mukhtar Robow.

Tangu mwaka 2006 kundi la Al-Shabab limekuwa likitekeleza mashambulzi kadhaa ya bomu hasa mjini Mogadishu,Kampala Uganda na Nairobi nchini Kenya na kusababisha vifo vya maelfu ya watu.

Kundi hili bado linathibiti Kusini kwa Somalia lakini wanajeshi wa Umoja wa Afrika, wanaojumuisha wale kutoka Ethiopia na Kenya wamefaulu kuchua tena uthibiti wa miji hiyo huku wanajeshi kutoka Uganda na Burundi wakithibiti mji mkuu Mogadishu.

Aidha,majeshi ya Kenya yamefaulu kuthibiti wa mji wa Afmado na sasa wanalenga kuchukua uthibiti wa mji wa Kismayu ambao ndio ngome kubwa ya Al-Shabab.

Serikali ya mpito nchini Somalia inatarajiwa kumaliza muda wake tarehe 20 mwezi Agosti mwaka huu na hivyo uchaguzi mkuu unatarajiwa kuandaliwa kuchagua serikali mpya.

Hali ya usalama nchini Somalia imedorora tangu mwaka 1991 wakati utawala wa rais wa zamani Mohamed Siad Barre ulipomalizika.
 

tags: Kenya - Kundi la Wanamgambo la Al Shabab - Marekani - Somalia - Uganda
MAELEZO
Tuma maoni yako kwa makala haya
Maudhui ya eneo hili yatakuwa ya kibinafsi na kuto kuonyeshwa kwa watu wote.
To prevent automated spam submissions leave this field empty.
CAPTCHA
Swali hili ni kwa ajili ya kupima kama wewe si roboti ili kuzuia spam ya papo kwa papo.
Close