Rais Assad atamba wapinzani wake hawawezi kushinda kwenye mapigano yanayoendelea kwenye nchi hiyo
Rais Bashar Al Assad amesema wapiganaji wa upinzani hawawezi kuibuka washindi kwenye mapigano ambayo yanaendelea kwa miezi kumi na nane nchini Syria dhidi ya jeshi lake lakini amesisitiza mlango wa mazungumzo bado upo wazi. Assad amekwenda mbali na kusema wapinzani nchini Syria wamekuwa wakipanga na kutekeleza vitendo vya kigaidi ndani ya jamii zao lakini hahawezi kufanikiwa kwenye vita yao ya kutaka kuiangusha serikali yake.
Kauli ya Rais Assad imekuja saa kadhaa baada ya watu hamsini na wanne kupoteza maisha nchini Syria baada ya helkopta waliyokuwa wanasafiria kuanguka kwenye kituo cha mafuta katika Jimbo la Al Riqqa.
Assad akiwa Damascus amewaambia wapiganaji wa upinzani mabadiliko katika nchi hiyo hayawezi kutokea kwa msaada wa uvamizi wa majeshi ya nje kama ambavyo wamekuwa wakiomba msaada kwa mataifa ya magharibi.
Kiongozi huyo wa Syria amesema pande zote ambazo zinasigana zipo sawa na suluhisho pekee ni kurejea kwenye meza ya mazungumzo ili kumaliza machafuko ambayo yameendelea kushuhudiwa na kuchangia umwagaji wa damu.
Mpatanishi wa mgogoro wa Syria Lakhdar Brahimi alipokutana na Rais Assad juma lililopita alisema hali nchini Syria inazidi kuwa na mbaya na lazima hatua haraka zichukuliwe kukabiliana nayo.
Kiongozi huyo wa Syria amesema kuna makosa yalifanyika nchini mwake na huenda yakawa sababu ya kutokea kwa machafuko yanayoendeshwa na wapinzani wakishinikiza mabadiliko ya utawala.
Rais Assad licha ya kuzungumzia suala la machafuko katika nchi yake lakini amekiri viongozi wa serikali yake wamekuwa wakijihusisha na ulaji wa rushwa unaochangia utendaji mbovu.
Machafuko ya miezi kumi na minane nchini Syria yamesababisha vifo vya watu zaidi ya elfu ishirini na tisa huku Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani UNICEF likitoa ripoti inayoonesha ukiukwaji wa haki za watoto.







MAELEZO
Tuma maoni yako kwa makala haya