Pata taarifa kuu
SYRIA-MASHAMBULIZI

Syria: Juhudi za kukomesha machafuko Aleppo

Juhudi za Urusi zimekua zikiendelea Jumapili hii kwa ajili ya ukomeshaji wa uhasama katika jimbo la Aleppo, wakati ambapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry anatazamiwa kuwasili mjini Geneva, kwa mazungumzo ya dharura kuhusu maafa yasiyo na kifani nchini Syria.

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria Staffan de Mistura Machi 14, 2016 Geneva.
Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria Staffan de Mistura Machi 14, 2016 Geneva. PHILIPPE DESMAZES/AFP
Matangazo ya kibiashara

Baada ya mashambulizi ya usiku yaliofanywa na pande mbili husika katika mgogoro huo, serikali kwa upande mmoja na waasi kwa upande mwengine, hali ya utulivu imeshuhudiwa Jumapili hii katika mji wa Aleppo (kaskazini), lakini mitaa ilikua patupu, raia wamejizuia kutoka nje kwa hofu ya mashambulizi mapya, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.

Wakazi kadhaa wa maeneo yanayodhibitiwa na waasi walikimbia siku ya Jumamosi mashambulizi ya anga ya serikali katika mji wa pili wa nchi hiyo, ambao umekuwa uwanja mkuu wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoingia mwaka wake wa sita sasa.

Urusi ambayo ni mshirika wa karibu wa Bashar al-Assad, imitangaza kuwa mazungumzo yamekua yakiendelea ili kufikia kusimamishwa kwa mapigano katika jimbo la Aleppo, baada ya wito wa Marekani wa kuitaka serikali ya Syria kukomesha mashambulizi katika mji mkuu wa jimbo hilo.

"Kwa sasa, mazungumzo ya kweli yanaendelea ili kuanzisha 'mfumo wa ukimya' katika jimbo la Aleppo," amesema jenerali Sergei Kouralenko, akinukuliwa na vyombo vya habari vya Urusi.

Siku moja kabla, Moscow ilisema kuwa haitoiomba serikali ya Syria kusitisha mashambulizi yake katika jimbo la Aleppo, ikibaini kwamba ni "mapambano dhidi ya tishio la kigaidi."

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani, Papa Francis, Jumapili hii, ametoa wito kwa pande zote nchini Syria kuheshimu mkataba wa usitishwaji wa mapigano.

Jimbo la aleppo liliopo kwenye mpaka na Uturuki, limegawanyika kati ya serikali, waasi, Wakurdi na wanajihadi, kundi la Islamic State (IS).

Wakati mchakato wa amani ukiendelea kukabiliwa na changa moto nyingi john Kerry anatarajiwa kuwasili mjini Geneva kujadili na mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Syria, Staffan de Mistura, na wenzake wa Saudi Arabia, Jordan kuhusu mkataba wa usitishwaji wa mapigano na mabadiliko ya kisiasa katika jaribio la kumaliza vita vilivyogharimu maisha ya watu zaidi ya 270,000 tangu mwaka 2011.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.