Pata taarifa kuu
CECAFA-TFF-TANZANIA-KAGAME CUP

CECAFA yatoa ratiba ya michuano ya kombe la Kagame 2015

Baraza la vyama vya soka kwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati CECAFA, juma hili limetoa ratiba rasmi ya michuano ya kombe la Kagame kwa mwaka 2015, michuano ambayo itafanyika jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Kutoka kushoto, katibu mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye, wa pili kutoka kushoto, Leodegar Tenga, rais CECAFA na Jamal Malinzi, rais wa TFF
Kutoka kushoto, katibu mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye, wa pili kutoka kushoto, Leodegar Tenga, rais CECAFA na Jamal Malinzi, rais wa TFF RFIKiswahili
Matangazo ya kibiashara

Akuzungumza Jumatano ya wiki hii jijini Dar es Salaam, Tanzania, rais wa CECAFA Leodegar Tenga, amesema kuwa mashindano ya mwaka huu yanatarajiwa kufana kutokana na kuzialika timu ambazo wanaamini ni mabingwa katika nchi zao.

Tenga ameongeza kuwa michuano ya mwaka huu inatoa fursa kwa vilabu vinavyoshiriki kuonesha wachezaji wao kimataifa kwakuwa ni michuano ambayo itaoneshwa na kituo cha Super Sport cha Afrika Kusini.

Rais Tenga ametumia fursa hiyo kuviomba vilabu hivyo kuja na timu zao za kwanza na sio kuleta timu B ambazo hazitaleta ushindani kwenye mashindano haya mengine makubwa barani Afrika.

Kwa upande wake, katibu mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye amesema kuwa maandalizi yote yamekamilika na wanaishukuru Serikali ya Tanzania pamoja na shirikisho la mpira nchini humo kukubali kuwa mwenyeji wa michuano ya mwaka huu.

Aidha Musonye amesema kuwa kutokana na kukosekana kwa mdhamini mkuu, timu zitakazoshiriki michuano ya mwaka huu zitajigharamia safari za kutoka kwenye nchi zao hadi Tanzania huku suala la malazi na usafiri wa ndani ukifadhiliwa na nchi mwenyeji.

Musonye amesema timu zimegawanywa katika makundi matatu, ambapo kutakuwa na kundi A, kundi B na kundi C.

Kundi A, litakuwa na timu za Yanga kutoka Tanzania, Gor Mahia kutoka Kenya, Telecom kutoka Djibouti, KMKMΒ kutoka Zanzibar na Khartoum National kutoka Sudan, katika kundi hili Musonye anasema timu tatu zitatinga kwenye hatua ya robo fainali.

Kundi B, litakuwa na timu za APR kutoka Rwanda, Al-Ahly Shendi kutoka Sudan, Lydia Ludic kutoka Burundi pamoja na Hegan FC ya Somalia, kwenye kundi hili timu mbili zitafuzu kwenda hatua ya robo fainali.

Kundi C, litakuwa na timu za Azam FC ya Tanzania, Malakia kutoka Sudan Kusini, Adama City kutoka Ethiopia pamoja na KCCA kutoka Uganda, kwenye kundi hili pia timu mbili ndizo zitakazofuzu hatua ya robo fainali.

Mashindano ya kombe la Kagame, yanadhaminiwa na rais wa Rwanda Paul Kagame ambaye hutoa zaidi ya dola elfu 50 kudhamini michuano hii mikubwa ya vilabu kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.