Kenya: Waislam zaidi ya 150 watuhumiwa ugaidi
Jeshi la polisi nchini Kenya limesema kuwa litawafikisha mahakamani zaidi ya watu 150 kwa tuhuma za kushirikiana na kundi la kigaidi la Al Shabab. Operesheni polisi ya kuwasaka wafuasi wa kundi hilo inaendelea katika misikiti kadhaa inayodaiwa kutoa mafunzo ya itikadi kali za kidini katika mji wa Mombasa.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Cheza - 02:24
Katika operesheni ya polisi ya hivi karibuni katika Misikiti mbalimbali mji Mombasa, watu 250 walikamatwa wakituhumiwa kushirikiana na kundi la Al Shabab linaloendesha harakati zake nchini Somalia.
Watuhumiwa hao walifikishwa Mahakamani, lakini watuhumiwa 91 waliachiliwa huru kwa kukosekana ushahidi wa kutosha.
Hata hivyo watuhumiwa wengine zaidi ya 150 bado wanazuiliwa jela. Polisi nchini Kenya imesema itawafungulia mashtaka watuhumiwa hao kwa kosa la kushirikiana na kundi la Al Shabab.
Mashirika yanayotetea haki za binadamu nchini Kenya yamesema kwamba watu hao wanaozuiliwa jela hawana hatia yoyote, bali ni mbinu za utawala za kutaka kuendelea kuwakandamiza baadhi ya watu kutoka jamii ya Waislam.
Kenya imekua ikishuhudia mashambulizi ya mara kwa mara tangu rais Uhuru Kenyatta achukuwe hatamu ya uongozi wa nchi. Kundi la Al Shabab limekua likinyooshewa kidole kuhusika na mashambulizi hayo.
Viongozi tawala wamewataka raia kushirikiana na polisi ili kuwafichua wahalifu hususan watu wanaoshirikiana na makundi ya kigaidi kwa lengo la kuimarisha usalama wa taifa.