Pata taarifa kuu
RWANDA-BURUNDI-UHASAMA-USHIRIKIANO-USALAMA

Paul Kagame: “viongozi wa Burundi wahatarisha usalama wa raia wao”

Baada ya miezi kadhaa serikali ya Burundi kuitwika lawama Rwanda kuwa ndio inachochea vurugu nchini Burundi kwa ushirikiano na maafisa kadhaa waliokimbilia nchini Rwanda baada ya kushindwa jaribio la mapinduzi May 13, hatimaye Rwanda umetoka katika ukimya na kubaini kwamba machafuko yanayoendelea Burundi yanasababishwa na viongozi wenyewe.

Rais wa Rwanda Paul Kagame (mwanzo) na Rais Pierre Nkurunziza (nyuma).
Rais wa Rwanda Paul Kagame (mwanzo) na Rais Pierre Nkurunziza (nyuma). AFP PHOTO/JOSE CENDON
Matangazo ya kibiashara

Rais wa Rwanda ameinyooshea kidole cha lawama serikali ya Burundi kuwa ndio inahusika na mauaji ya raia wake, huku akisema akisisitiza kuwa serikali imeshindwa kuwalindia usalama raia wake. Ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Kigali nchini Rwanda Ijumaa Novemba 6.

Rais Kagame amesema ni jambo lisilokubalika kuona miili ya watu waliouawa ikitupwa barabarani, katika mito na maziwa, huku akibaini kwamba hali inayojiri Burundi wakati huu inatisha.

Rais wa Rwanda amesema viongozi wa Burundi wangelipaswa kujifunza kupitia mauaji ya kimbari yaliotokea nchini mwake mwaka 1994, ambayo baadhi ya viongozi walio madarakani wakati huu nchini Burundi walihusika.

“ Burundi imefungia misaada au imeanza kufungiwa misaada kutokana na hali inayofanana na ile iliyotokea hapa. Serikali inaua watu asubuhi hadi jioni. Rais mwenyewe haonekani, amejificha, nchi inaongozwa na na rais asiyekuwepo. Seriali ya Burundi ikijifunza kwa yale yaliyotokea hapa nchini Rwanda mwaka 1994, mauaji ambayo baadhi ya viongozi walio madarakani nchini Burundi walihusika. Kwa hiyo viongozi wa Burundi wanatabia mbaya, na hawawajibiki kwa kuwalindia usalama raia wao. Mimi najiuliza kila mara sisi waafrika na tuna kasumba gani kwa raia wetu? Kwa hiyo sisi wanayarwanda tunapaswa kujitenga na maovu ya aina yoyote, kwa kuepukana na yale yaliyotokea hapa nchini ”, amesema Rais Paul Kagame.

“ Viongozi wote wa Burundi wanadai kuwa wanaabudu, wanamjuwa Mungu, na kuna baadhi ambao ni wachungaji, Mungu wanaomkubali na kumjua ni wa wapi” Mungu gani huyo anaye amuru viongozi kuwaua na kuwaangamiza raia wao. Wanadai kwamba wanatembea kila mahali na biblia, wapi Biblia inaamuru viongozi kuua raia wao? Ipo biblia hiyo ”, ameuliza Rais wa Rwanda.

Hayo yakijiri watu tisa wameuawa usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili hii katika eneo la Busoro wilayani Kanyosha, Kusini mwa jiji la Bujumbura. Zaidi ya watu ishirini wamejeruhiwa katika shambulizi hilo. Mashahidi wamebaini kuwa watu waliokua wamevalia sare ya polisi ndio wamehusika na mauaji hayo. Mauaji hayo yametokea katika baa moja ilio karibu na kituo cha polisi.

Hata hivyo polisi imesema kuwa imeanzisha unchunguzi ili kujua waliohusika na shambulio hilo. Lakini imetupilia mbali madai kwamba polisi ndio imehusika na mauaji hayo.

Mauaji hayo yanatokea wakati muda uliokua umetolewa na Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza akiwataka wakazi wa maeneo ambayo ni kitovu cha maandamano dhidi ya muhula wake wa tatu wanaomiliki silaha wajisalimishe, umetamatika usiku wa manane Jumamosi Novemba 7, 2015.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kwa ombi la Ufaransa, litakutana Jumatatu Novemba 9 kujadili hali mbaya inayoendelea Burundi pamoja na kauli za kuchochea mauaji ziliyotolea wiki hii na viongozi wa nchi hiyo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.