Pata taarifa kuu
ZIMBABWE

Mahakama Zimbabwe yaagiza mke wa Mugabe kurejesha ardhi aliyopokonya wanakijiji

Mahakama kuu ya Zimbabwe imetoa agizo kuzizuia mamlaka za Serikali ya nchi hiyo kuwadhalilisha wanakijiji wanaodaiwa kuwa kwenye ardhi ya shamba ya mke wa rais wa Mugabe, Grace Mugabe.

Mke wa rais wa Zimbabwe, Grace Mugabe.
Mke wa rais wa Zimbabwe, Grace Mugabe. Zanu-PF/handout
Matangazo ya kibiashara

Mke wa rais Mugabe, anataka kuligeuza shamba hilo kuwa kituo cha uhifadhi wanyamapori.

Jaji Felistus Chatukuta amemuagiza waziri wa ardhi na makazi Douglas Mombeshora na waziri wa mambo ya ndani Ignatius Chombo pamoja na kamishna wa polisi Augustine Chihuri kuacha mara moja kubomoa nyuma za wanakijiji hao wala kuwaondoa.

Wanakijiji hao waliwaomba mawakili kutoka shirika la kutetea haki za binadamu nchini humo, kufungua kesi kwenye mahakama kuu wakitaka mahakama iagize polisi kuacha kuwanyanyasa na kuwaonea wanakijiji hao walio kwenye shamba la Arnold mjini Mazowe kwenye jimbo la Mashonaland ambako wameishi kwa zaidi ya miaka 17.

Serikali yenyewe ndio iliwakubalia wanakijiji hao kufanya makazi kwenye shamba hilo mwaka 2000 wakati Serikali ilipoanza kutekeleza sera ya utaifishaji wa radhi kutoka kwa wazungu na kuwapa wazawa.

Mzozo kati ya wanakijiji hao na mke wa rais Mugabe, ulianza kushika kasi mwaka 2015 baada ya Grace Mugabe ambaye anamiliki eneo kubwa la shamba hilo kuanza mchakato wa kufungua hifadhi ya wanyamapori.

Hata hivyo Polisi nchini Zimbabwe wamekuwa wakitumia nguvu kuwahamisha wanakijiji hao toka mwaka 2015 wakikaidi amri halali ya mahakama iliyotolewa mwaka huo huo.

Kwenye kesi yao wanakijiji hao waliiomba mahakama iagize Polisi kusitisha unyanyasaji ambapo familia kadhaa mpaka sasa zimeachwa bila makazi baada ya nyumba zao kubomolewa na watoto wao wako hatarini kuacha shule.

Mahakama kuu imeagiza kuwa maofisa wa Polisi na wale wa Serikali kutoka kwenye wizara ya ardhi na makazi kuheshimu haki za wanakijiji hao dhidi ya kuondolewa kwa nguvu na kwamba wanayo haki za usiri na kimili ardhi kwenye nchi yao.

Hii ni mara ya pili kwa mamlaka za Zimbabwe kuagizwa na mahakama kuu kuacha kuwanyanyasa wanakijiji wa Mazowe, kuvunja nyumba zao na kuwaondoa kwa nguvu.

Uamuzi mwingine wa mahakama uliosema hatua ya mke wa rais kuwaondoa kwa nguvu wanakijiji hao ulikuwa batili ni ule uliotolewa mwaka 2015.

Grace Mugabe, ambaye anaaminika kuwa na nia ya kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu ujao, pia ameendelea kukaidi agizo la mahakama kurejesha ardhi aliyochukua kwa wanakijiji hao ambayo aliichukua kwa nguvu kutoka kwa mfanyabiashara wa Lebanon baada ya kutofautiana nae kuhusu biashara ya pete waliyokuwa wakifanya kwenda mrama.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.