Pata taarifa kuu
DRC-KABILA

DRC: Chama cha upinzani UDPS chakutana kuchagua mgombea urais

Chama kikuu cha upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kinafanya mkutano wake mkuu wa siku mbili ulioanza Ijumaa hii kwa lengo la kuchagua mtu ambaye atakuwa mgombea wake kwenye uchaguzi mkuu wa mwezi Desemaba.

Wafuasi wa chama kikuu cha upinzani nchini DRC.
Wafuasi wa chama kikuu cha upinzani nchini DRC. Junior KANNAH / AFP
Matangazo ya kibiashara

Miongoni mwa vinara wa chama cha UDPS wanaopewa nafasi ya kupewa kibarua hicho ni pamoja na Felix Tshisekedi mtoto wa aliyekuwa muasisi wa chama hicho Etienne Tshisekedi ambaye alifariki dunia jijini Brussels, mwezi Februari mwaka jana.

Uchaguzi mkuu wa DRC umepangwa kufanyika tarehe 23 ya mwezi Desemba mwaka hu baada ya kuahirishwa kwa zaidi ya mara mbili na kusababisha kuzuka kwa maandamano na hofu ya machafuko.

Rais Joseph Kabila amekuwa madarakani tangu mwaka 2001 na alitakiwa kuondoka madarakani mwishoni mwa mwaka 2016 baada ya kumaliza mihula yake miwili kikatiba.

Hata hivyo anasalia madarakani kwa kutumia kipengele cha katiba kinachomtaka rais kutoka madarakani pale mrithi wake anapokuwa amechaguliwa.

Mvutano kuhusu kuendelea kusalia madarakani kwa rais Kabila kumesababisha maandamano makubwa yaliyosababisha watu kadhaa kupoteza maisha na wengine mamia kujeruhiwa.

Kwa mujibu wa kura ya maoni iliyotolewa Ijumaa hii, imeonesha kuwa asilimia 69 ya watu hawana imani na tume ya uchaguzi CENI kuandaa uchaguzi huku asilimia 80 wanamtazamo hasi na rais Kabila.

Kura hiyo imeongeza kuwa asilimia 66 watapiga kura kwa kinara wa upinzani wakati rais Kabila angepata asilimia 6 ya kura ikiwa angewania tena kiti hicho.

Miongoni mwa vinara wa upinzani ambao  ni maarufu yumo Moise Katumbi gavana wa zamani wa Katanga ambaye aliungwa mkono na asilimia 24 ya waliotoa maoni yao.

Anafuatiwa na Tshisekedi aliyepewa asilimia 13.

Katumbi ambaye kwa sasa anaishi uhamishoni, alitangaza rasmi kuwa atawania urais wa nchi hiyo Machi 12 mwaka huu ambapo pia alizindua vuguvugu lake la kisiasa aliloliita "Pamoja kwa Mabadiliko."

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.