Pata taarifa kuu

Mazungumzo kati ya makundi ya waasi na serikali yaendelea Nairobi

Mazungumzo ya amani , kati ya makundi ya waasi nchini DRC isipokuwa wale wa M23 ambao hawakualikwa, wawakilishi wa serikali na viongozi wa  mashirika ya kiraia, yanaingia siku ya pili leo jijini Nairobi, baada ya kufunguliwa hapo jana na viongozi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Rais wa Kenya William Ruto anazindua mazungumzo ya tatu yanayojumuisha makundi mbalimbali ya waasi na serikali kutoka DRC Jumatatu, 29 Novemba mjini Nairobi.
Rais wa Kenya William Ruto anazindua mazungumzo ya tatu yanayojumuisha makundi mbalimbali ya waasi na serikali kutoka DRC Jumatatu, 29 Novemba mjini Nairobi. © RegionWeek
Matangazo ya kibiashara

Jana, rais wa Uganda Yoweri Museveni akizungumza kwa njia ya vídeo alisema silaha kuendelea kusalia mikononi mwa makundi ya waasi, kunaendelea kuzorotesha usalama Mashariki mwa DRC, huku Paul Kagame wa Rwanda akisema wakati umefika wa kumaliza kabisa mgogoro Mashariki mwa nchi hiyo. 

Rais Museveni amefahamisha kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki inatakiwa kubuni mipango mikakati katika kuhakikisha mzunguuko wa silaha hizo kinyume cha sheria unadhibitiwa ili kuhakikisha amani ya kudumu na usalama zinapatikana mashariki mwa DRC.  

"Tatizo kubwa ni silaha haramu nchini DRC, silaha hizi zimekuwepo tangu nchi hiyo ilipopata uhuru wake, na silaha hizo ziko mikononi mwa makundi ya kigeni yenye silaha, " alisema rais wa Uganda. 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais wa Burundi Évariste Ndayishimiye, amewaambia raia wa DRC kuwa mazungumzo kati yao ndio njia pekee ya kupatikana kwa suluhu ya mgogoro unaolikumba taifa hilo, kauli ambayo pia imesisitizwa na mratibu wa mazungumzo ya amani aliyeteuliwa na Jumuiya hiyo ya Afrika Mashariki na Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta  

Miongoni mwa makundi yaliyoshiriki mazungumzo haya hivi leo ni pamoja na kundi la CODECO kutoka Mkowa wa Ituri, ambapo msemaji wa kundi hilo amesema kile wao wamekuja kuomba ni msamaha wa serikali ya DRC.  

Viongozi wa nchi wanachama wa EAC waliohudhuria pia mkutano kwa njia ya mtandao ni pamoja na Felix Tshisekedi wa DRC, Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda. Mazungumzo haya yameanza siku ya Jumatatu,  huku yakitarajiwa kumalizika mnamo Dsemba 3 mwaka huu. 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.