Pata taarifa kuu

RCA: ICC yachunguza mashtaka mengi dhidi ya mwanamgambo wa zamani Maxime Mokom

Katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), vikao vya uthibitisho wa mashtaka dhidi ya Maxime Mokom vinaanza Jumanne hii, Agosti 22. Akichukuliwa na mwendesha mashtaka kama mkuu wa zamani wa operesheni za kijeshi za kundi la wanamgambo wa Kikristo la Anti-Balaka, Maxime Mokom anashitakiwa kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita uliofanywa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati mwaka 2013 na 2014.

Makao makuu ya ICC huko Hague, Uholanzi.
Makao makuu ya ICC huko Hague, Uholanzi. © Wikimédia
Matangazo ya kibiashara

Na mwanahabari wetu huko Hague, Stéphanie Maupas

Siku tatu za vikao zitamuwezesha mwendesha mashtaka kupata hati ya mashtaka ya mshukiwa aliyefungwa tangu mwezi Machi 2022.

Hivyo, itakuwa imechukua miezi kumi na saba, tangu kukamatwa kwa Maxime Mokom nchini Chad, ili Mahakama iweze kufanya vikao hivi. Mara kadhaa katika miezi ya hivi karibuni, majaji pia walizingatia kwamba mtuhumiwa anapaswa kuachiliwa kwa dhamana lakini, hadi leo, hakuna nchi inayokubali kumuwekwa chini ya kizuizi cha nyumbani kwenye ardhi yake wakati kesi yake ikisubiriwa ... bado ni mbali sana kuona ufunguzi wa kesi yake.

Mwanamgambo huyo wa zamani, mwenye umri wa miaka 44, anasalia gerezani. Kwa sasa, mwendesha mashtaka lazima apate kutoka kwa majaji uthibitisho wa mashtaka, ambayo ni makosa ishirini ya mauaji, ubakaji, uporaji na mateso.

Changamoto ngumu zaidi kwa mwendesha mashtaka itakuwa kushawishi kwamba Maxime Mokom alipanga mashambulizi huko Bangui na Bossangoa, Desemba 2013, kutoka Zongo, nchini DRC, ambako alikuwa mkimbizi. Upande wa mashtaka pia unadai kwamba alifadhili kwa kiasi kikubwa kundi la wanamgambo wa Kikristo la Anti-Balaka kwa pesa kutoka mfukoni mwake, lakini pia kwa kuomba pesa kutoka kwa familia ya rais wa zamani François Bozizé, ambaye ni mshirika wake wa karibu.

Maxime Mokom pia alikuwa Waziri wa Upokonyaji Silaha kwa muda mfupi baada ya makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mjini Khartoum, mwaka wa 2019, kabla ya kuchukua tena silaha.

Mwishoni mwa vikao hivyo, Alhamisi, Agosti 24, majaji watakuwa na miezi miwili kuthibitisha au la mashtaka dhidi yake.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.