Pata taarifa kuu
USALAMA-ULINZI

Mali: Watu kadhaa wauawa katika mashambulizi ya ndege zisizo na rubani Kidal

Jeshi la Mali limefanya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani Jumanne asubuhi, Novemba 7, 2023, mjini Kidal. Takriban watu kumi wameuawa, wakiwemo watoto wawili hadi wanne, kulingana na vyanzo, na karibu ishirini kujeruhiwa: idadi ambayo inaweza kuongezeka.

Kidal, kaskazini mwa Mali, mnamo 2020.
Kidal, kaskazini mwa Mali, mnamo 2020. AFP - SOULEYMANE AG ANARA
Matangazo ya kibiashara

Kidal, kaskazini mwa Mali, ni kitovu cha vita kati ya jeshi la Mali na kundi  la waasi wa CSP, ambalo Kidal ni ngome yake. Kiini cha vita hivi: kambi ya kikosi cha wanajeshi wa Umoja wa Mataifa, MINUSMA, iliyochukuliwa na waasi wa CSP wiki moja iliyopita, baada ya kuondoka kwa walinda amani wa mwisho, na ambayo jeshi linakusudia kuichukuwa. Hii ndio kambi ambayo ililengwa asubuhi ya leo.

Mabomu matatu ndani ya chini ya saa moja: Bomu la kwanza lilianguka karibu na kambi, karibu saa 9:00 kwa saa za Mali, bomu la pili lilianguka ndani ya kambi, na la tatu katika njia ya kutoka kaskazini-mashariki ya jiji.

Kulingana na vyanzo vilivyohojiwa na RFI, watoto waliouawa nje ya kambi hiyo walikuwa wakicheza wakati wa mapumziko na kutafuta vitu vya kuchezea.

Raia kadhaa pia waliuawa katika mashambulozi haya, akiwemo kiongozi wa jamii, afisa wa mamlaka ya muda ya Kidal, kiongozi wa kampuni moja...

CSP inahakikisha kwamba hakuna wapiganaji wake kati ya waathirika.

Kwa ombi la RFI, jeshi la Mali halikujibu na halijawasiliana rasmi katika hatua hii.

Kambi ya Umoja wa Mataifa tayari ilikuwa ikilengwa na ndege zisizo na rubani siku tatu zilizopita, ambazo hazikusababisha hasara yoyote.

Jeshi la Mali na washirika wake kutoka kundi la wanamgambo wa Urusi Wagner wanakusudia kuiondoa CSP kutoka kambi ya Umoja wa Mataifa ili kuimiliki.

Wakihojiwa na RFI, wakaazi wa Kidal hawafichi hofu zao mbele ya tishio hili la angani. "Hakuna aliye salama," alisema jana mkaazi mmoja wa Kidal ambaye aliitaka familia yake kukimbilia Algeria.

Katika taarifa zao kwa vyombo vya habari hivi karibuni, jeshi la Mali na waasi wa CSP wametoa wito kwa watu kuondoka katika maeneo ya mapigano.

Huko Kidal, maeneo yaliyo hatarini zaidi ni uwanja wa ndege na kambi za kijeshi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.