Pata taarifa kuu

DRC: Idadi kubwa ya vikosi vya ulinzi vyatumwa Lubumbashi, hofu yatanda kwa wakazi

Siku tano baada ya Uchaguzi Mkuu nchini DRC, wanajeshi  wengi wametumwa mjini Lubumbashi, ngome ya Moïse Katumbi, mpinzani mkuu wa Rais anayemaliza muda wake Félix Tshisekedi. Hali ambayo inatia wasiwasi zaidi wakaazi katika jiji hili la shaba. Mamlaka, kwa upande wao, wanahakikisha kwamba jeshi limetumwa ili kuhakikisha usalama unalindwa vilivyo katika kipindi hiki cha sikukuu za mwishomwa mwaka.

Moja ya barabara za mji wa Lubumbashi, Desemba 22, 2023.
Moja ya barabara za mji wa Lubumbashi, Desemba 22, 2023. AFP - PATRICK MEINHARDT
Matangazo ya kibiashara

Na mwanahabari wetu mjini Lubumbashi, Denise Maheho

Tangu siku ya Jumapili, makumi ya wanajeshi kutoka kikosi cha walinzi wa Jamhuri wameonekana katika maeneo kadhaa ya kimkakati huko Lubumbashi, hasa katikati mwa jiji, kwenye uwanja wa ofisi ya posta, kwenye kituo cha redio na televisheni vya taifa (RTNC) na kwenye lango la kaskazini la jiji….Wakiwa na silaha nyingi, askari hawa huzunguka katika mitaa kadhaa. Hali ambayo inamtia wasiwasi Gislain Kalwa, kiongozi wa shirika la kiraia katika eneo hilo:

"Uwepo uliyoimarishwa wa wanajeshi unazua hofu na kuzua maswali. Nini kinaendelea?Kwa nini kupeleka askari wengi? Hofu inazidi kuongezeka na hii inaleta hofu.”

Kwa upande wake, Meya wa Jiji, Martin Kazembe, amewatolea wito raia kutokuwa na hofu yoyote:

“Hao ni askari wetu. Wapo ili kuhakikisha usalama. Wanatimiza tu kazi yao ya kawaida wakati wa sikukuu hizi za mwisho wa mwaka. Raia wa Lubumbashi wanatakiwa kuendesha shughuli zao kwa amani."

Vyanzo vingine vinaamini kuwa idadi hii kubwa ya wanajeshi imetumwa ili kuzuia vurugu zozote kutoka upande wa wafuasi wa Moïse Katumbi kufuatia kuchapishwa kwa sehemu ya matokeo ya uchaguzi wa urais.

Wakati jeshi, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari siku ya Jumapili, likishutumu kituo cha televisheni cha Nyota, kilicho karibu na Katumbi, kwa kutangaza habari zinazoelekea kuwavunja moyo na kuwavuruga wanajeshi, kituo hiki kilifutilia mbali shutuma hizo dhidi yake.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.