Rwanda yakanusha madai ya kushambulia kambi ya wakimbizi nchini DRC
Rwanda imekanusha madai ya Marekani kuwa, wanajeshi wake walishambulia kwa mabomu kambi ya wakimbizi ya Mugunga Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kusababisha vifo vya watu tisa siku ya Ijumaa asubuhi.
Imechapishwa:
Hatua hii ya Rwanda inakuja baada ya Marekani kupitia Wizara ya Mambo ya nje, kulaani mashambulio hayo na kuwalaumu wanajeshi wa Rwanda na waasi wa M 23 kwa kuhusika.
Msemaji wa serikali ya Rwanda, Yolande Makolo, katika taarifa aliyoichapisha kwenye ukurasa wake wa X, amekanusha madai hayo na kuwatuhumu waasi wa FDLR na Wazalendo, aliosema wanaungwa mkono na serikali na jeshi la DRC kwa kurusha mabomu hayo.
Aidha, amesema wanajeshi wa Rwanda ni weledi na hawazi kuwalenga na kuwashambulia wakimbizi.
This is ridiculous Matthew, how do you come to this absurd conclusion? The RDF, a professional army, would never attack an IDP camp. Look to the lawless FDLR & Wazalendo supported by the FARDC, for this kind of atrocity. https://t.co/vtyawZLxBp
— Yolande Makolo 🇷🇼 (@YolandeMakolo) May 4, 2024
Kutokana na mashambulio hayo, rais Felix Thsisekedi ambaye anazuru barani Ulaya amesema anasitisha ziara yake nchini Hungary ili kurejea nyumbani, kushughulikia changamoto hiyo.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alipokutana na rais Thsisekedi jijini Paris, aliitaka Rwanda kuacha kuwaunga mkono waasi wa M 23 na kuwaondoa wanajeshi wake mashariki wma DRC.
Haya yanajiri wakati huu waasi wa M 23 wanaoripotiwa kuungwa mkono na Rwanda, wakiendelea kuchukua maeneo kadhaa jimboni Kivu Kaskazini, wiki hii walifanikiwa kuudhibiti mji wenye utajiri wa madini wa Rubaya.