Pata taarifa kuu

Msumbiji: Chama tawala FRELIMO chamchagua kiongozi wake ajaye

Chama tawala nchini Msumbiji, FRELIMO, kimemchagua gavana wa mkoa wa Inhambane, Daniel Chapo, kama kiongozi wake mpya: atamrithi Rais Filipe Nyusi ikiwa chama hicho kitashinda uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi wa Oktoba, chama hicho kimetangaza usiku wa Jumapili kuamkia Jumatatu.

Daniel Chapo, Gavana wa mkoa wa Inhambane, Msumbiji.
Daniel Chapo, Gavana wa mkoa wa Inhambane, Msumbiji. RFI/Orfeu Lisboa
Matangazo ya kibiashara

Kamati kuu ya FRELIMO yenye wajumbe wapatao 250, imemchagua Bw. Chapo dhidi ya wagombea wengine watatu wa ndani, katika uamuzi wa mshangao uliotangazwa baada ya midahalo mikali ya zaidi ya siku mbili, kura kadhaa mfululizo na hatimaye kujitoa kwa mpinzani wake wa karibu.

Daniel Chapo, profesa wa zamani wa sayansi ya siasa na mtangazaji wa redio, amekuwa gavana wa mkoa wa kati wa Inhambane tangu mwaka 2016. Akiwa na umri wa miaka 47, ndiye mgombea urais wa kwanza wa FRELIMO kuzaliwa baada ya uhuru kutoka Ureno mwaka 1975.

"Kwa kuchaguliwa kwa mgombea wake wa urais, FRELIMO imechukua hatua muhimu kujiandaa kwa ushindi wake katika uchaguzi wa Oktoba," Rais Nyusi alisema Jumapili usiku, akifunga kongamano lisilo la kawaida la chama tawala karibu na mji mkuu Maputo.

FRELIMO imeshinda kila uchaguzi wa kitaifa tangu uhuru na pia inadhibiti idadi kubwa ya mamlaka za mikoa na mitaa. Katiba inamzuia Nyusi, 65, kuwania muhula wa tatu Oktoba 9, wakati wananchi wa Msumbiji pia watakapochagua bunge lao na mamlaka za majimbo.

Nyusi aliitaka FRELIMO "kumpa uungwaji wetu wote mkono Daniel Chapo", baada ya uchaguzi wa ndani ambao ulishuhudia mpinzani wa karibu wa Chapo, Roque Silva, anayeonekana kuwa mrithi wa asili wa Nyusi, kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho dakika za mwisho na kujiuzulu nafasi yake ya Katibu Mkuu wa FRELIMO. Bw. Chapo aliahidi kuwa mgombea wa umoja. Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kongamano hilo, aliahidi "kufanya kazi na kila watu wote, vijana, wanawake, wanaume na maveterani."

Ushindi wa kishindo wa FRELIMO katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2019 ulipingwa na chama kikubwa zaidi cha upinzani, RENAMO, kundi la zamani la waasi. RENAMO na FRELIMO walipigana vita vya wenyewe kwa wenyewe (1977-1992) ambavyo viliharibu uchumi na kusababisha vifo vya karibu watu milioni moja.

mMwezi Oktoba mwaka jana, watu kadhaa waliuawa wakati wa maandamano makubwa ya kulaani matokeo yaliyochukuliwa kuwa yameibiwa katika chaguzi za mitaa. Polisi waliwafyatulia risasi waandamanaji katika miji kadhaa. RENAMO, ikikemea ulaghai na kudai ushindi mjini Maputo, ilitoa mwito wa maandamano baada ya FRELIMO kutangazwa mshindi katika manispaa 64 kati ya 65 zilizopambaniwa.

Nchi hiyo ilikuwa imeweka matumaini makubwa katika hifadhi kubwa ya gesi asilia iliyogunduliwa katika ufuo wa jimbo la kaskazini la Cabo Delgado mwaka 2010. Lakini vita vya msituni vilivyoanzishwa tangu mwaka 2017 na makundi ya wanajihadi wenye silaha wanaohusishwa na kundi la Islamic State vimesitisha uchimbaji wa gesi hiyo. Zaidi ya watu 5,000 wameuawa na karibu milioni moja wamelazimika kukimbia makazi yao tangu ghasia kuanza.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.