Pata taarifa kuu
LIBYA-UFARANSA

Viongozi wa Dunia kuijadili Libya nchini Ufaransa wakati watoto wa Kanali Gaddafi wakitoa taarifa zinazokinzana

Viongozi wa Dunia wanatarajiwa kukutana hii leo nchini Ufaransa katika Jiji la Paris kujadili hatima ya nchi ya Libya baada ya kuangushwa kwa Utawala wa Kanali Muammar Gaddafi na kuanza kwa uongozi mpya chini ya Baraza la Mpito la Waasi NTC.

Reuters/Esam Al-Fetori
Matangazo ya kibiashara

Viongozi wanaotarajiwa kukutana ni pamoja na wawakilishi kutoka Ufaransa wakiongozwa na Rais Nicolas Sarkozy, Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton.

Mkutano huo umepewa jina la “Marafiki wa Libya” unatarajiwa kuibuka na njia za kuhakikisha Baraza la Mpito la Waasi litatawala kwa misingi inayofaa badala ya ile ambayo ilikuwa awali.

Kabla ya kuanza kwa Mkutano huo tayari nchi ya Urusi imeingia kwenye kundi la mataifa ambayo yamewakubali Waasi kama watawala wapya wa Libya taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje mapema asubuhi ya leo imethibitisha.

Mkutano huo wa Viongozi unakuja wakati ambapo kumeibuka kauli mbili zinazosigana kutoka kwa watoto wa Kanali Gaddafi kwani kuna moja inayosisitiza kuendelea kwa mapigano wakati nyingine inataka upatanishi.

Seif Al-Islam mtoto wa Kanali Gaddafi ambaye anatajwa kuwa mtetezi mkubwa wa Baba yake ametoa ujumbe akisema wanajeshi watiifu kwa serikali ya baba yake wataendelea kupambana na Waasi hadi tone lao la mwisho la damu.

Seif Al-Islam akizungumza kutoka Tripoli amesema Utawala wao upo sawa na hata Kiongozi wa nchi hiyo yupo salama na kutoa onyo kali kwa Waasi ambao wanaendelea kufanya mashambulizi katika Mji wa Sirte.

Mtoto huyo wa Kanali Gaddafi amewahakikishia wananchi wa Libya kwamba wapo bado wapo katika nchi hiyo na wataendelea kukabilia na Waasi ambao wanataka kuuangusha Utawala wao.

Katika hatua nyingine Mtoto mwingine wa Kanali Gaddafi, Saadi Gaddafi amesema ujumbe ambao amepewa na baba yake ni wa kumtaka kurejesha mapatano badala ya kuendelea na mapigano yaliyosababisha vifo vya mamia ya wananchi.

Kauli ya Saadi inaonekana kukinzana na ile ya Seif Al-Islam ambaye yeye ameendelea kusisitiza watapigana hadi mwisho na wala hakuna mtu ambaye atarudi nyuma kwenye kipindi hiki.

Kutofautiana huku kwa kauli kuna kuja wakati ambapo Waasi kupitia Makamu Mwenyekiti wao Mahdi Al-Harati akitangaza kukamatwa kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Kanali Gaddafi, Abdelati Al-Obeidi.

Naye Msemaji wa Majeshi ya Waasi Kanali Ahmed Omar Bani amesema kwa sasa wanajiandaa kwa shambulizi la mwisho kabla ya kuiweka mikononi nchi yote na kisha Utawala wao uanze kazi.

Mapigano nchini Libya yamedumu kwa kipindi cha zaidi ya miezi sita ambapo Waasi waliweza kusonga mbele kwa kusaidiwa na mashambulizi ya Majeshi ya Kujihami ya Nchi za Magharibi NATO.

Machafuko na mapigano hayo yalikuwa ni muendelezo wa kufanya mabadiliko ya utawala yaliyoanzia nchini Tunisia na kumuangusha Zine Al Abidine Ben Ali na kisha kutua nchini Misri na kumuondoa Hosni Mubarak.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.