Pata taarifa kuu
DRC-UGANDA-TANZANIA

Mawaziri wa Ulinzi kutoka ICGLR waunda Tume ya Kijeshi itakayolichunguza Kundi la Waasi la M23 linaloshambulia Mashariki mwa DRC

Mawaziri wa Ulinzi wa Nchi Wanachama za Ukanda wa Maziwa Makuu ICGLR wamekubaliana kuunda Tume ya Kijeshi ambayo itafanya kazi ya kulichunguza Kundi la Waasi la M23 ambalo linapambana na Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC katika eneo la Mashariki.

Kikosi cha Wapiganaji wa Kundi la M23 wakishangilia walipofanikiwa kulitwaa eneo la karibu na Jimbo la Kivu Kaskazini
Kikosi cha Wapiganaji wa Kundi la M23 wakishangilia walipofanikiwa kulitwaa eneo la karibu na Jimbo la Kivu Kaskazini REUTERS/James Akena
Matangazo ya kibiashara

Uamuzi huo wa Mawaziri kumi na moja wanachama wa ICGLR umefikiwa walipokutana huko Mjini Goma nchini DRC ambapo kila nchi wanachama itawajibika kutoa wanajeshi wawili kwa ajili ya kushiriki kwenye Tume hiyo ya Uchunguzi ambayo itafanyakazi yake kwa kipindi cha mwezi mmoja.

Tume hiyo itaanza kazi yake mapema tarehe ishirini na mbili ya mwezi Septemba ikiwa chini ya wanajeshi wa Tanzania wakiwa na kibarua kikubwa cha kuchunguza kazi ambazo zinafanywa na Kundi la Waasi la M23 sambamba na operesheni zao zote katika eneo la Mashariki la DRC.

Waziri wa Ulinzi wa Uganda Crispus Kiyonga amesema kazi ya Tume hiyo ya Uchunguzi itakuwa ni kufahamu ukubwa wa kikosi cha Kundi la Waasi la M23 pamoja na zana ambazo wanamiliki sambamba na eneo ambalo wanalishikilia hadi sasa ili kujua wao watakuwa na kazi kiasi gani.

Waziri Kiyonga amesema Kundi la Waasi la M23 lazima likubali kuchunguzwa kama ambavyo Mawaziri wa Ulinzi kutoka ICGLR walivyokubaliana na iwapo watakaidi amri hiyo watashambuliwa na kuondolewa kwenye maeneo ambayo wamekuwa wakiyashikilia hadi sasa.

Kwa upande wake Gavana wa Kivu Kaskazini Julien Paluku amesema Tume hiyo ya kijeshi itapata ulinzi kutoka Jeshi la DRC linalotambulika kama FARDC sambamba na Kikosi cha Umoja wa mataifa Kinacholinda Amani nchini humo MONUSCO ili kuhakikisha wanatekeleza shughuli zao kama ilivyopangwa.

Gavana Paluku ameongeza kuwa kazi ya Tume hiyo ya Uchunguzi ya Kijeshi ni kuhakikisha wanaanda mazingira bora ambayo yatasababisha kuundwa kwa kikosi kisichoegemea upande mmoja ili kulinda mipaka ya Mashariki mwa DRC inayoshambuliwa na kundi la M23.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.