serikali ya Bahrain yatangaza kuunda tume ya wanasheria kupitia hukumu zilizotolewa na mahakama
Serikali ya Bahrain kwa mara ya kwanza imetangaza kuunda tume maalumu ya wanasheria kwa ajili ya kupitia upya baadhi ya hukumu ambazo zimetolewa na mahakama za kijeshi kufuatia maandamano ya mwaka uliopita.
Imechapishwa:
Hatua hiyo imetokana na mapendekezo ya tume maalumu iliyoundwa na serikali mwaka jana kuchunguza mauaji yanayotuhumiwa kutekelezwa na polisi wakati wa maandamano ya kuupinga utawala wa nchi hiyo.
Mpaka sasa mahakama za kijeshi nchini humo zimetoa hukumu tano za watu kunyongwa hatua iliyolazimu tume hiyo kuundwa kuchunguza uhalali wa hukumu hizo na watu wanaoendelea kushikiliwa kwenye magereza mbalimbali nchini humo.
Mwishoni mwa mwaka jana tume maalumu iliyoundwa na mfalme Hamad-Bin-Isa-Al-Khalifa ilikabidhio ripoti yake na kubainisha kuwa polisi walitumia nguvu kubwa katika kukabiliana na waandamanaji huku pia ikieleza kuwa kuna wanaharakati wanashikiliwa kimakosa na polisi.
Serikali ya marekani hivi karibuni ilisema kuwa itaiuzia silaha za kijeshi nchi hiyo kulingana na utekelezaji wa mapendekezo ya tume iliyoundwa na serikali kuchunguza vurugu za nchini humo.