Pata taarifa kuu
SHERIA-HAKI

Al-Jazeera kuchukua hatua za kisheria na kupambana 'hadi mwisho' kufuatia uamuzi wa Israel

Mkurugenzi wa habari wa Al-Jazeera English ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kituo chake kitatumia njia zote zinazowezekana za kukata rufaa kupinga kisheria kufungwa kwa ofisi yake nchini Israel na kitapambana "hadi mwisho".

Makao makuu ya Al-Jazeera huko Doha, Qatar.
Makao makuu ya Al-Jazeera huko Doha, Qatar. © Kamran Jebreili / AP
Matangazo ya kibiashara

Siku ya Jumapili, serikali ya Israel iliamua kufunga ofisi ya Al-Jazeera nchini Israel, na kusababisha kukatizwa kwa matangazo ya televisheni. Uamuzi huo unatumika kwa muda wa siku 45, kulingana na hati rasmi.

"Waandishi wa Al-Jazeera walidhoofisha usalama wa Israeli na kuchochea ghasia dhidi ya wanajeshi wa Israeli," alieleza Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.

Umoja wa Mataifa ulishutumu "uamuzi unaorudisha nyuma uhuru wa vyombo vya habari", na nchi kadhaa, haswa Marekani, mshirika mkuu wa Israel, zilipinga uamuzi huu.

"Ikiwa kuna uwezekano wa kupinga uamuzi huu, tutatumia njia zote," Salah Najm alisema siku ya Jumatatu.

Muda mfupi baada ya uamuzi wa serikali ya Israel, sehemu ya vifaa vya idhaa hiyo vilikamatwa vikiwemo vifaa vyake vya utangazaji. Pia iliondolewa kutoka kwa waendeshaji satelaiti na kebo, na tovuti zake zilizuiwa.

"Vifaa vilivyochukuliwa, hasara ambayo tulipata kwa sababu ya kusitishwa kwa matangazo yetu, yote haya ni suala la hatua za kisheria," amesisitiza mkurugenzi wa habari wa Al-Jazeera English, akikosoa uamuzi "unaostahili miaka ya 1960 badala yake kuliko karne ya 21".

Leo, kwenye skrini za idhaa za Kiarabu na Kiingereza za Al-Jazeera, ujumbe kwa Kiebrania unaonekana ukisema "imesitishwa nchini Israeli."

- "Uamuzi wa kiholela" -

Kituo hiki cha Qatar mara moja kililaani uamuzi huo wa serikali ya Israel, na kuuita "uhalifu" na kutangaza kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba "umekiuka haki ya kupata habari."

Salah Najm pia ameuita uamuzi wa kufungwa kwa ofisi ya Al-Jazeera "uamuzi wa kiholela."

Lakini alipuuzia athari za kufungwa kwake kwa sababu kituo hiki kinaweza kutegemea vyanzo vingine vya habari kwa kukosekana "watu walio nchini Israel", amesema.

"Ninajua watu ambao wana VPN (mtandao wa kibinafsi ) wanaweza kutuona mtandaoni wakati wowote," mkurugenzi amesema.

Al-Jazeera pia inaendelea kufanya kazi katika Ukingo wa Magharibi, eneo la Palestina linalokaliwa na Israeli tangu mwaka 1967, na katika Ukanda wa Gaza, ambapo inaendelea kutangaza moja kwa moja juu ya vita kati ya Israeli na Hamas, ambayo ilianza Oktoba 7 baada ya shambulio lisilo na kifani la Hamas katika ardhi ya Israel.

Uamuzi huo wa Israel unakuja baada ya Bunge la Israel, Knesset, kupiga kura mapema mwezi Aprili kwa sheria ya kupiga marufuku matangazo ya vyombo vya habari vya kigeni nchini Israel ambavyo vinadhoofisha usalama wa taifa, sheria inayolenga kituo hiki cha Qatar, ambayo inamuwezesha Waziri Mkuu kupiga marufuku utangazaji wa vyombo vya habari vinavyolengwa na kufunga ofisi zake.

Sababu kuu ya mvutano wa historia kati ya Al-Jazeera na Israel: kifo cha mwandishi wake wa habari Mmarekani mwenye asili ya Palestina Shireen Abu Akleh wakati wa uvamizi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, Mei 2022. Al-Jazeera inaishutumu Israel kwa kumuua kimakusudi.

- Mateso na kutoaminiana -

Tangu kuanza kwa vita katika Ukanda wa Gaza, ofisi ya Al-Jazeera katika ardhi ya Palestina imeshambuliwa kwa mabomu na waandishi wake wawili wameuawa.

Mkuu wa ofisi hiyo, Waël al-Dahdouh, alijeruhiwa na shambulio la Israel mnamo mwezi wa Desemba, ambalo liliua mpigapicha wa kituo hicho.

"Al-Jazeera ilipoteza baadhi ya watu, familia zao ziliteseka, jambo ambalo ni tofauti sana na migogoro mingine kwa maana hii," amelalamika Bw. Najm.

Kwa mujibu wa Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari (CPJ), shirika leenye makao yake makuu mjini New York, waandishi wa habari wasiopungua 97 wameuawa tangu kuanza kwa vita kati ya Israel na Hamas Oktoba 7, wakiwemo Wapalestina 92.

Vifo vya waandishi wa habari “sio jambo ambalo tunaweza kulizungumzia kwa upole,” amesema Bw. Najm.

"Lazima tuwe waangalifu, tuwe waangalifu na kuwahadharisha watu kuhusu hali ya vita vinavyoendelea na jinsi ambavyo ni hatari kwa watu na kwetu kama taaluma," ameongeza.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.