Pata taarifa kuu

Mashambulizi Rafah: Marekani yasitisha kuipa mabomu Israeli

Wiki iliyopita, Marekani ilisitisha utoaji wa shehena ya mabomu ya pauni 2,000 na 500 baada ya Israel kushindwa kujibu "wasiwasi" wa Washington kuhusu mashambulizi yaliyotangazwa dhidi ya mji wa Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza, ametangaza afisa wa ngazi ya juu katika serikali ya Marekani.

Wataalamu wa silaha hushughulikia bomu la JDAM kwenye sitaha ya shehena ya ndege kubwa ya Marekani "Abraham Lincoln". Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani pia inatathmini uhamisho wa aina hii ya silaha kwa Israel.
Wataalamu wa silaha hushughulikia bomu la JDAM kwenye sitaha ya shehena ya ndege kubwa ya Marekani "Abraham Lincoln". Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani pia inatathmini uhamisho wa aina hii ya silaha kwa Israel. AFP - PHILIP MCDANIEL
Matangazo ya kibiashara

“Tulisimamisha utoaji wa shehena ya silaha wiki jana. Inajumuisha mabomu 1,800 ya pauni 2,000 (kilo 907) na mabomu 1,700 ya pauni 500 (kilo 226)," ametangaza, afisa mkuu wa utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden kwa sharti la kutotajwa jina. "Hatujafanya uamuzi wa mwisho kuhusu jinsi ya kuendelea na usafirishaji huu," aliongeza.

Haja ya mpango wa kuaminika

Uamuzi huu ulichukuliwa huku Washington ikipinga mashambulizi makubwa yaliyotayarishwa na wanajeshi wa Israel huko Rafah. Marekani imeweka wazi kuwa haiungi mkono mashambulizi bila ya kuwa na mpango wa kuaminika wa kuwalinda raia waliokimbilia katika mji huo. Joe Biden "alisisitiza msimamo wake" kwa Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu Jumatatu, Mei 6.

Maafisa wa Israeli na Marekani wamejadili njia mbadala, lakini "majadiliano haya yanaendelea na hayajashughulikia kikamilifu wasiwasi wetu," afisa mkuu wa Marekani pia amesema. "Wakati viongozi wa Israeli walionekana kuunga mkono uamuzi juu ya operesheni kama hiyo, tulianza kuchunguza kwa uangalifu mapendekezo ya kuhamisha silaha maalum kwa Israeli ambazo zinaweza kutumika huko Rafah. Zoezi hili lilianza mwezi Aprili,” afisa huyu mkuu ameeleza.

Uhamisho mwingine wa silaha unachunguzwa

Afisa huyo wa ngazi ya juu katika serikali ya Marekani anaongeza kuwa Washington "ililenga haswa" katika kutumia mabomu mazito zaidi ya pauni 2,000 "na athari ambayo inaweza kuwa nayo katika mazingira ya mijini kama vile tumeona katika sehemu zingine za Gaza". Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani pia inatathmini uhamisho mwingine wa silaha, ikiwa ni pamoja na matumizi ya mabomu ya usahihi yanayojulikana kama JDAM, afisa huyo ameongeza.

Israel ilituma vifaru siku ya Jumanne, Mei 7, huko Rafah (kusini), ilichukua udhibiti wa kivuko cha mpaka na Misri na kufunga sehemu kuu mbili za kufikia misaada ya kibinadamu (Rafah na Kerem Shalom), hatua inayochukuliwa kuwa "isiyokubalika" na Marekani. Jeshi la Israel linaongeza mashambulizi ya anga. Mapema leo Jumatano, Mei 8, mashahidi wameripoti mashambulizi katika maeneo tofauti kwenye ardhi ya Palestina, haswa katika mji wa Gaza (kaskazini) ambapo hospitali ya al-Ahli imetangaza vifo vya watu saba wa familia moja katika shambulio la angani.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.