Pata taarifa kuu

Israeli yatekeleza mashambulio Gaza baada ya wapatanishi kuondoka Cairo

Israel imeripotiwa kutekeleza mashambulio mpya katika ukanda wa Gaza, hatua inayokuja baada ya wapatanishi wa mzozo unaoendelea mashariki ya kati kuondoka mjini Cairo bila ya kuafikia makubaliano.

Israeli imeapa kuendelea na mpango wake wa kutekeleza oparesheni za kijeshi mjini Rafah kwa kile inachosema ni kuwalenga Hamas.
Israeli imeapa kuendelea na mpango wake wa kutekeleza oparesheni za kijeshi mjini Rafah kwa kile inachosema ni kuwalenga Hamas. AFP - -
Matangazo ya kibiashara

Mashambulio haya ya mapema leo Ijumaa, yanakuja wakati huu ambapo Misri nchi mojawapo wa wapatanishi wa mzozo wa Gaza, ikisema ni lazima Hamas na Israeli walegeze misimamo iwapo wanahitaji kuafikia suluhu la kusitisha mapigano pamoja na kubadilishana wafungwa.

Mapigano kati ya pande hizo mbili yameingia  katika mwezi wa saba sasa licha ya wito wa jamii ya kimataifa wa kutaka muafaka kuafikiwa mara moja.

Katika mawasiliano ya njia ya simu kati ya waziri mkuu wa Misri na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken, wanadiplomasia hao wamekubaliana kutumia njia zote zilizopo kuhakikisha suluhu ya kinachoendelea inapatikana.

Mamia ya raia wa Palestina wameondoka kusini mwa Gaza baada ya Israeli kuwataka kuondoka kuelekea oparesheni zake za kijeshi. Tarehe 9 Mei 2024.
Mamia ya raia wa Palestina wameondoka kusini mwa Gaza baada ya Israeli kuwataka kuondoka kuelekea oparesheni zake za kijeshi. Tarehe 9 Mei 2024. AP - Abdel Kareem Hana

Haya yanajiri wakati huu wapiganaji wa Hamas wakieleza kwamba wapatanishi wake wamelazimika kuondoka mjini Cairo kunakofanyika mazungumzo ya kupata suluhu kuelekea mjini Doha kwa madai kuwa Israeli imekataa mapendekezo yake.

Tayari Hamas imesisitiza kuwa iko tayari kutekeleza mapendekezo yake kuhusu usitishaji wa mapigano na kwa kwamba jukumu limesalia mikononi mwa Israeli kufanya uamuzi wake.

Soma piaGaza: Wajumbe wa Hamas na Israel waondoka Cairo, juhudi za upatanishi 'zinaendelea'

Nalo shirika la habari linalohusishwa na serikali ya Misri Al-Qahera limeripoti kwamba, wapatanishi wa Israeli nao pia wameondoka mjini Cairo.

Katika taarifa ya wizara ya mambo ya kigeni ya Misri, mazungumzo hayo yako katika hatua ya mwisho na iwapo Israeli itatekeleza uvamizi katika mji wa Rafah wenye idadi kubwa ya raia basi hatua hiyo huenda ikatishia usalama na uthabiti wa ukanda huo.

Kwa upande wake, msemaji wa wizara ya ndani ya Marekani Matthew Miller, ameeleza kwamba, Waziri Blinken alimhakikishia Shoukry kwamba Washington haiuungi mkono mpango wa Israeli kutekeleza oparesheni za kijeshi huko Rafah.

Tayari waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema nchi yake itatekeleza operesheni kwenye mji wa Rafah, hata kama mshirika wake wa karibu Marekani, atasitisha msaada wa silaha kwa nchi hiyo.

"Mara nyingi tumekuwa tukikubaliana na rais wa Marekani Joe Biden ambaye tumejuana kwa miaka mingi sana lakini wakati mwengine tunakosa kukubaliana." amesema Benjamin Netanyahu.

00:40

Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu

Kundi la Hamas lilikubali rasimu ya makubaliano ya usitishaji mapigano juma hili, likisema uamuzi uko kwa Israel ikiwa inataka Amani kwenye eneo la Gaza.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.