Pata taarifa kuu
MISRI

Sisi: Sitaingilia uamuzi wa Mahakama kuhusu hukumu ya Wanahabari wa Al Jazeera

Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi amesema hataingilia kati uamuzi wa Mahakama wa kuwahukumu wanahabari watatu wa Al Jazeera kukaa jela miaka saba kwa kosa la kutoa habari za kupotosha na kuwa wanachama wa kundi haramu lililopigwa marufuku la Muslim Brothehood.

Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi
Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi REUTERS/Egyptian Presidency/Handout via Reuters
Matangazo ya kibiashara

Kauli hii ya rais Al Sisi inakuja baada ya shinikizo za Jumuiya ya Kimataifa kutaka wanahabari hao kuachiliwa huru.

Rais huyo mpya amesema kuwa uongozi nchini humo unaheshimu sheria za na uhuru wa Mahakama.

“ Hatutaingilia maamuzi ya Mahakama,” Sisi alisisitiza wakati wa hotuba kwa wanajeshi siku ya Jumanne jijiji Cairo.

“ Ni lazima tuheshimu maamuzi ya Mahakama na sio kuyakosoa hata kama wengine hawaelewi uamuzi huo,” alisisitiza.

Rais wa Misri  Abdel Fattah  al-Sissi kulia na Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry
Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sissi kulia na Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry REUTERS/Brendan Smialowski/Pool

Shinikizo zinaendelea kutolewa kwa serikali ya Misri kuwaachilia huru wanahabari hao Peter Greste raia wa Australia, Mohamed Fadel Fahmy na Baher Mohamed wameendelea kukanusha tuhma dhidi yao.

Waandishi wengine 11 wa Al-Jazeera ambao hawakuwa Mahakamani nao walihukumiwa jela miaka 10, wakiwemo Wanahabari wawili kutoka Uholanzi na Uingereza.

Awali, Australia ilisema inawasiliana moja kwa moja na serikali ya Misri kuiomba kuwaachilia huru Wanahabari hao ambao inasema wao walikwenda tu kufanya kazi yao na hawana ushirikiano na kundi la Muslim Brotherhood.

Waziri wa Mambo ya nje wa Australia Julie Bishop naye amesema kesi hizo zilichochewa kisiasa na serikali ya Misri imeshindwa kuthibitisha kuwa wanahabari hao walitekeza makosa hayo.

Naye Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry amelaani hukumu hiyo na kuongeza kuwa Marekani pia inazungumza na rais Abdel Fattah al-Sisi kumwomba kuwaachilia huru wanahabari hao.

Wanahabari wa Al-Jazeera wakiwa Mahakamani
Wanahabari wa Al-Jazeera wakiwa Mahakamani REUTERS/Asmaa Waguih

Familia za wanahabari hao wamesema kuwa watakata rufaa kuhakikisha kuwa ndugu zao wanaachiliwa huru na kurudi nyumbani.

Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa Navi Pillay naye pia ameshutumu hukumu hiyo ambayo amesema ni ukiukwaji wa haki za binadamu na uhuru wa waandishi wa Habari duniani.

Mataifa kadhaa barani Ulaya yamesema yatawahoji Mabalozi wa Misri katika nchi zao kuhusu hukumu iliyotolewa dhidi ya wanahabari hao.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.