Sudan: Mariam al-Mahdi aachiliwa huru
Shirika la habari la SUNA nchini Sudan - limesema mwanasiasa mmoja mashuhuri wa upinzani ameachiwa huru baada ya kushikiliwa kwa mwezi mmoja.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Shirika hilo la habari limesema naibu mwenyekiti wa chama cha upinzani cha Umma, Mariam Sadek al-Mahdi, ameachiwa huru jumanne wiki hii.
Alikuwa korokoroni kwa muda wa siku 28 katika jela ya wanawake la Omdurman, baada ya vikosi vya usalama kumkamata katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Khartoum Agosti 11 iliyopita.
Alikuwa akirejea nyumbani kutoka Paris ambako alikuwa na mazungumzo ya kusaka umoja pamoja na wapinzani wa rais Omar al-Bashir.
Baba yake Sadek al-Mehdi, mwenyekiti wa chama cha upinzani cha Umma, Sadek al Mehdi pia alikamatwa mapema mwaka huu baada ya kuvilaumu vikosi vya serikali kuhusika na visa vya ukiukaji wa haki za binaadamu katika jimbo la Darfur, kufuatia kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2003.