Pata taarifa kuu
KENYA-MGOMO-ELIMU

Kenya: Rais Kenyatta awaweka wazi waalimu

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amelihutubia taifa Jumapili wiki hii, akisema kinagaubaga kuwa serikali ya nchi hiyo haina uwezo wa kulipa nyongeza ya mishahara wanayodai waalimu wanaoendelea na mgomo.

Rais wa Kenya, akiwasisitizia waalimu kuwa serikali yake haina uwezo wa kulipa nyongeza ya mishahara wanayodai waalimu.
Rais wa Kenya, akiwasisitizia waalimu kuwa serikali yake haina uwezo wa kulipa nyongeza ya mishahara wanayodai waalimu. Kenyagvt
Matangazo ya kibiashara

Rais Kenyatta ametolea wito wadau wote wa elimu nchini Kenya kuketi kwenye meza ya mazungumzo kwa faida ya taifa na wanafunzi ili kuweza kutafutia suluhu mgogoro huo, ambao ametaka utatuliwe kwa amani na kusema kuwa shule zote zinafungwa kuanzia lJumatatu wiki hii.

Wiki iliyopita serikali ya Kenya iliamuru shule zote nchini Kenya zifungwe kuanzia leo Jumatatu.

Hata hivyo mgomo wa walimu unaendelea kushuhudiwa nchini humo, huku ukiathiri mambo mengi ikiwa ni pamoja na kushuka kwa kiwango cha elimu kwa wanafunzi na wengi kwa sasa wamekua wakiranda randa hovyo mitaani.

Barua kutoka kwa wizara ya elimu iliagiza hivi karibuni shule zote za umma na za kibinafsi zifungwe na wanafunzi warudi nyumbani.

Wanafunzi wanaojiandaa kufanya mitihani ya kitaifa ya darasa la nane na kidato cha nne mwaka huu ndio watasalia shuleni pekee.

Chama cha walimu nchini Kenya KNUT kimefahamisha kuwa tayari kimepokea barua hiyo ya kufungwa kwa shule kutoka kwa serikali kuanzia jumatatu wiki hii.

Hivi karibuni muungano wa upinzani nchini Kenya CORD uliwaambia viongozi wao katika Bunge la kitaifa na lile la Senate kuandaa mswada wa kukosa imani na rais wa nchi hiyo Uhuru Kenyatta.

Wanasiasa wa upinzani walisema walichukua hatua hiyo kwa sababu rais Kenyatta ameshindwa kuiheshimu Katiba na kutii amri ya Mahakama ya kuitaka serikali kuwalipa walimu ili kumaliza mgomo unaoendelea.

Wiki iliyopita chama cha walimu wa shule za sekondari kilimtumia barua Spika wa bunge la kitaifa kuitisha kikao cha dharura kujadili suala la mgomo huu wa walimu.

Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta amesema haina pesa za kuwaongezea walimu mshara, huku Wizara ya elimu ikisema mitihani ya kitaifa ya darasa la Nane na Kidato cha nne itaendelea kama ilivyopangwa, na uzinduzi wake ulifanyika Ijumaa wiki iliyopita.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.