Pata taarifa kuu
USALAMA-ULINZI

Uasi wa M23 nchini DRC: Wanajeshi wa Uganda kutumwa mwishoni mwa mwezi Machi

Baada ya Wakenya na Warundi, wanajeshi wa Uganda kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wataanza kutumwa mwishoni mwa mwezi Machi katika maeneo yanayokaliwa kwa sasa ya Mashariki mwa DRC na waasi wa M23, afisa wa Uganda amesema Alhamisi.

Wanajeshi wa Kenya wakiwasili Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Novemba 16, 2022, kama sehemu ya operesheni ya kijeshi ya kikanda inayolenga waasi katika eneo hilo.
Wanajeshi wa Kenya wakiwasili Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Novemba 16, 2022, kama sehemu ya operesheni ya kijeshi ya kikanda inayolenga waasi katika eneo hilo. © RFI/Florence Morice
Matangazo ya kibiashara

"Wanajeshi wetu watakwenda Bunagana, Rutshuru, Mabenga na Kiwanja", Kanali Mike Walaka Hyeroba ametangaza huko Goma, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini, ambaye alikuja kukutana na mamlaka ya kijeshi ya mkoa huo. "Wataanza kutumwa mwishoni mwa mwezi huu," ameongeza afisa huyo, bila kutaja idadi yao.

Jeshi la Uganda lilitangaza mwezi Novemba kwamba lilikuwa karibu kutuma wanajeshi 1,000 kama sehemu ya kikosi hiki. Maeneo yaliyotajwa na kanali wa Uganda yanapatikana katika eneo la Rutshuru, kaskazini mwa Goma, ambapo M23 imechukua maeneo makubwa tangu mwaka jana. Mji wa Bunagana, kitovu cha kibiashara kwenye mpaka wa Uganda, ulianguka mikononi mwa waasi hao mnamo Juni 13, 2022.

Katika eneo hilo, wanajeshi wa Kenya kutoka katika kikosi cha EAC wametumwa tangu mwisho wa 2022, ambao tayari wanashutumiwa na wananchi kwa kutowalazimisha waasi kuondoka, bali kuishi pamoja nao.

Wanajeshi wa Burundi kutoka EAC, kwa upande wao, wametumwa katika eneo jirani la Masisi, kaskazini magharibi mwa Goma, ambako mapigano bado yameripotiwa siku ya Alhamisi. Mwishoni mwa mwezi Desemba, jeshi la Sudan Kusini lilitangaza kutuma "haraka iwezekanavyo" wanajeshi 750, ambao bado hawajafika katika eneo hilo.

Kundi la M23 ni waasi wa zamani ambao wengi wao ni Watutsi, ambao walichukua silaha tena mwishoni mwa mwaka 2021 na, kulingana na wataalam wa Umoja wa Mataifa, wanaungwa mkono na Rwanda. Mipango kadhaa ya kidiplomasia hadi sasa imeshindwa kutatua mzozo huo. EAC iliamua mwezi Juni mwaka jana kuunda kikosi cha kijeshi, sambamba na mipango hii na pamoja na kikosi cha Umoja wa Mataifa (MONUSCO), kwa lengo la kuleta amani Mashariki mwa Kongo, eneo linalokubwa na ghasia za silaha kwa karibu miaka 30.

Wanajeshi wa Uganda tayari wamekuwepo nchini DRC tangu mwishoni mwa mwaka 2021, si kama sehemu ya kikosi cha EAC bali kwa operesheni za pamoja zilizofanywa na jeshi la DRC dhidi ya waasi wenye asili ya Uganda, ADF (Allied Democratic Forces) . Operesheni hizi zinafanyika katika sehemu ya kaskazini ya mkoa wa Kivu Kaskazini na pia katika jimbo jirani la Ituri.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.