Pata taarifa kuu
SYRIA-UFARANSA-USWISS

Jeshi la Syria limefanikiwa kurejesha kwenye himaya yake Mkoa wa Qusayr uliokuwa unashikiliwa na Wapinzani

Jeshi la Syria limefanikiwa kuuweka kwenye himaya yake kwa mara ya kwanza Mkoa wa wa Qusayr unaopatikana katika mpaka wa nchi hiyo na Lebanon uliokuwa umeangukia kwenye mikono ya wapiganaji wa wapinzani. Televisheni ya Taifa ya Syria ndiyo imetangaza ushindi huo uliopatikana baada ya mapigano makali yaliyofanikisha kuwasambaratisha wapiganaji wa upinzani waliokuwa wanaushikilia mkoa huo kwa muda sasa.

Jeshi la Syria limefanikiwa kurejesha kwenye himaya yake Mkoa wa Qusayr uliokuwa unashikiliwa na Wapinzani
Jeshi la Syria limefanikiwa kurejesha kwenye himaya yake Mkoa wa Qusayr uliokuwa unashikiliwa na Wapinzani
Matangazo ya kibiashara

Taarifa zinaeleza kuwa Jeshi la Syria linalomtii Rais Bashar Al Assad limefanikiwa kuwaua magaidi wengi waliokuwa wanaushikilia Mkoa huo wa Qusayr uliopo katika Jimbo la Homs na kurejesha utawala wa serikali.

Ushindi huu kwa Jeshi la Syria ni mkubwa sana katika kipindi cha miezi ishirini na sita ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yenye lengo la kuuangusha Utawala wa Rais Assad unaokosolewa na Mataifa ya Magharibi.

Jeshi la Syria limeweza kurejesha Mkoa wa Qusayr kwenye himaya yake kutokana na kupata msaadamkubwa wa Wapiganaji wa Kundi la Hezbollah lenye maskani yake nchini Lebanon linaloisaidia Serikali ya Rais Assad.

Wanajeshi wa Serikali ya Syria walianzisha mkakati wa kuuchukua Mkoa wa Qusayr katika operesheni iliyoanza tarehe 19 ya mwezi Mei kabla ya kuongezewa nguvu na uwepo wa Wapiganaji wa Kundi la Hezbollah.

Ushindi huo wa Jeshi la Syria unakuja kipindi hiki viongozi kutoka Urusi, Marekani na wale wa Umoja wa Mataifa UN wanakutana Jijini Geneva kwa lengo la kufanya maandalizi ya kufanyika kwa mkutano wa serikali na wapinzani wa Damascus.

Mkutano huo unaandaliwa kipindi hiki ambacho utawala wa Damascus umeendelea kulaumiwa kwa kutumia silaha za kemikali kwenye mapigano yao dhidi ya wapinzani yaliyodumu kwa miezi ishirini na sita.

Serikali ya Ufaransa kupitia Waziri wa Mambo ya Nje Laurent Fabius imetangaza hakuna shaka yoyote kua Serikali ya Rais Assad inatumia silaha za kemikali kuwaua wananchi na hivyo wanashinikiza matumizi ya jeshi la Kimataifa ili kuweza kudhibiti umwagaji damu huo.

Tamko la Ufaransa linakuja siku moja baada ya Tume ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa UN kutoa taarifa yake inayoonesha wapinzani na serikali wote wanatumia silaha za kemikali pamoja na kufanya uhalifu dhidi ya binadamu.

Serikali ya Marekani kwa upande wake imesema licha ya kuwepo kwa taarifa hizo za Ufaransa lakini uchunguzi zaidi inabidi uendelee kufanyika ili kupata ushahidi wa kutosha ili kuweza kubaini kama kweli kuna matumizi ya silaha za kemikali.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Jay Carney amesema wao wataendelea kupinga matumizi ya silaha za kemikali kwenye machafuko yanayoendelea nchini Syria kwani yatachangia ongezeko la mauaji.

Uingereza nayo imesema serikali ya Rais Assad inapaswa kuwajibika kwa mauaji yanayoendelea kushuhudiwa nchini humo kauli ambayo imetolewa na Balozi wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa UN Mark Lyall Grant.

Takwimu za Umoja wa Mataifa UN zinaonesha watu zaidi ya 94,000 wamepoteza maisha katika machafuko yanayoendelea nchini Syria kwa zaidi ya miezi 26 huku maelfu ya wananchi wakilazimika kuomba hifadhi ya ukimbizi katika nchi jirani.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.