Pata taarifa kuu
SYRIA-MAREKANI-UFARANSA

Marekani yalaani Wanamgambo wa Hezbollah kulisaidia Jeshi la Syria kuchukua Utawala wa Mji wa Qusayr

Serikali ya Marekani imelaani kwa nguvu zake zote ushiriki wa Kundi la Wanamgambo wa Hezbollah kulisaidia Jeshi la Serikali linalomtii Rais Bashar Al Assad na kufanikiwa kuwafurusha wapinzani waliokuwa wanashinikia Mji wa Qusayr unaotajwa kuwa ni sehemu muhimu kimkakati. Washington imeituhumu serikali ya Rais Assad kutokana na kuwashirikisha Wanamgambo wa Hezbollah kwenye vita vinavyoendelea ndani ya nchi hiyo kitu kilichosaidia kupata ushindi na kurejea kwa utawala wao katika Mji wa Qusayr uliokuwa uanshikiliwa na Wapinzani kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Bendera ya Taifa ya Syria ikiwa imepandishwa kwenye mnara wa saa kuonesha kurejea kwa Utawala wa Serikali katika Mji wa Qusayr
Bendera ya Taifa ya Syria ikiwa imepandishwa kwenye mnara wa saa kuonesha kurejea kwa Utawala wa Serikali katika Mji wa Qusayr
Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa Ikulu ya Marekani maarufu kama White House Jay Carney ametoa wito wa kuwataka Wanamgambo wa Hezbollah na wanajeshi wa Iran wanaolisaidia Jeshi la serikali ya Syria kuondoka mara moja.

Taarifa hiyo ya Carney imeeleza Jeshi la Serikali ya Syria halina uwezo wa kuwasambaratisha wapinzani katika Mji wa Qusayr na wamefanikiwa kuurejesha kwenye himaya yao kutokana na msaada mkubwa walioupata kutoka kwa Wanamgambo wa Hezbollah.

Jeshi la Serikali ya Syria likisaidiwa na Wanamgambo wa Hezbollah walifanikiwa kuchukua utawala wa Mji wa Qusayr na kisha kusimika upya bendera ya serikali na kuanza zoezi la kufanya usafi ili kuruhusu barabara ziweze kutumika.

Jeshi la Serikali linatajwa kuwaua mamia ya wapiganaji wa wapinzani huku wengine wakijisalimisha kutokana na kuzidiwa kwenye mapambano yaliyodumu kwa siku kumi na saba na tayari wananchi wametakiwa kurejea kwenye makazi yao.

Mji wa Qusayr uliopo katika mpaka na Lebanon unatajwa kutumiwa kama njia kuu ya wapinzani kupitisha silaha zao kutoka mataifa ya magharibi ili waendelee kupambana na Jeshi la Serikali na kufurushwa kwao kunaashiria huenda wakawa na wakati mgumu kwenye mapigano hayo.

Haya yanakuja kipindi hiki Ufaransa ikiendelea kusisitiza Serikali ya rais Assad inatumia silaha za kemikali kwenye vita vyao dhidi ya wapinzani kauli inayopingana na ile iliyotolewa na Tume ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa UN iliyozitaja pande zote kutumia silaha hizo.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande amewaambia wanahabari wanaendelea kushiniukiza Jumuiya ya Kimataifa kuchukua hatua dhidi ya Utawala wa Rais Assad ambao wanajeshi wake wanatumia silaha za kemikali zilizopigwa marufuku.

Mapigano nchini Syria yanatarajiwa kuingia mwezi wa ishirini na saba ambapo takwimu za Umoja wa Mataifa UN zinaonesha watu 94,000 wamepoteza maisha huku maelfu wakiomba hifadhi ya ukimbizi katika nchi jirani.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.