Pata taarifa kuu

Viongozi wa ukanda wataka kusitishwa mapigano mashariki mwa DRC

Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, waliokutana hapo jana jijini Bujumbura Burundi, wamerudia tena wito wao wa usitishwaji mapigano kwa pande zote mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye, akiteta jambo na katibu mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dr Peter Mathuki. 04 / 02 / 2023
Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye, akiteta jambo na katibu mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dr Peter Mathuki. 04 / 02 / 2023 © Jumuiya
Matangazo ya kibiashara

Katika mkutano wao wa dharura ulioitishwa na mwenyekiti wa Jumuiya, rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye, viongozi walikubaliana kwa kauli moja, kutuma ujumbe wa kusitishwa haraka kwa mapigano.

Taarifa iliyotolewa na Jumuiya ya Afrika mashariki baada ya kikao hicho, imesema;

“Wakuu w anchi kwa kauli moja wamesisitiza mwito wao kwa pande zinazohusika kujiepusha na vurugu”.

Kauli yao imekuja siku chache kupita tangu waasi wa M23 waanze tena kurejea katika maeneo waliyotangaza kujiondoa mwezi mmoja uliopita, jimboni Kivu Kaskazini.

Mapigano kati ya M23 na jeshi la Serikali ya Congo, yamesababisha kuongezeka kwa mvutano wa mataifa jirani, ambapo DRC inaituhumu Rwanda kuwasaidia waasi hao.

Madai ya DRC, yaliungwa mkono na ripoti ya wataalamu wa umoja wa Mataifa, ambao katika ripoti yao, waliitaja moja kwa moja Rwanda kushirikiana na waasi hao, tuhuma ambazo Rwanda imekanusha.

Mkutano wa siku ya Jumamosi, ulikuwa ni muendelezo wa juhudia za kidiplomasia kujaribu kumaliza machafuko mashariki mwa DRC, ambayo yamesababisha watu zaidi ya laki 5 kukimbia makazi yao tangu Machi 2022.

Juma hili pia, kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis, alitembemea taifa hilo na kutoa wito wa amani na kukomeshwa machafuko, wito ambao hata hivyo umeonekana kuwa ni sikio la kufa.

Mwaka uliopita, viongozi wa ukanda waliokutana mjini Luanda, Angola, walifanikiwa kupata makubaliano yaliyoagiza kusitishwa kwa mapigano mashariki mwa DRC na kwa makundi ya waasi kuweka silaha chini, ikiwa ni pamoja na kuondoka katika maeneo waliyokuwa wanayakalia.

Hata hivyo licha ya maagizo hayo, kundi la waasi wa M23 limeendelea kukaidi maagizo hayo, ambapo limeondoka tu katika maeneo mchache huku likianza tena kurejea.

Hivi karibuni ripoti mpya ya umoja wa Mataifa, imelitaja kundi la M23 kukiuka makubaliano ya usitishaji mapigano na kuondoka katika maeneo wanayoyashikilia.

Katika taarifa ya Jumuiya, imeongeza kuwa;

“Makundi yote ya wapiganaji wa kigeni na makundi mengine kuondoka katika ardhi ya DRC, na kuwaagiza wakuu wa majeshi ya ukanda kukutana katika muda wa wiki moja, kujadili muda hali wa makundi hayo kujiondoa”

Aidha taarifa imewataka wakuu wa majeshi kupendekeza hatua zaidi za kuchukua ikiwa maelekezo yatakayotolewa hayatatekelezwa na makundi yenye silaha.

Januari 27 mwaka huu waasi wa M23, walichukua tena mji wa Kitshanga ulioko wilayani Masisi, na kushika barabara muhimu zinazounganisha eneo hilo na mji wa Goma.

Mkutano wa siku ya Jumapili, ulihudhuriwa na viongozi kutoka Rwanda, DRC, Uganda, Kenya, Tanzania na wenyeji Burundi.

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.