Pata taarifa kuu
KENYA-SIASA-UCHAGUZI

Heka heka zaanza kwa wanasiasa Kenya

Viongozi wakuu wa muungano wa upinzani nchini Kenya CORD, juma hili wote kwa pamoja wametangaza kuwa watapeperusha bendera za vyama vyao katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.

Raila Odinga, waziri mkuu wa zamani, ambaye ni kiongozi wa upinzan, Julai 7, 2014 Nairobi.
Raila Odinga, waziri mkuu wa zamani, ambaye ni kiongozi wa upinzan, Julai 7, 2014 Nairobi. REUTERS/Noor Khamis
Matangazo ya kibiashara

Hali hiyo inaashiria kuwa tayari kipenga kimelia kwa viongozi hao kuwania kupeperusha bendera ya muungano wao.

Chama cha FORD-Kenya chenyewe kimemteua Moses Wetangula kuwa mgombea wao, huku chama cha WIPER kikimteua kinara wake na makamu wa rais wa zamani Kalonzo Musyoka, wakati chama cha ODM chenyewe kikimteua kiongozi wa chama hicho na waziri mkuu wa zamani, Raila Odinga.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi hao wameapa kufanya uteuzi wa haki wa kuelekea kupata mgombea mmoja kati yao, atakayewania urais kwenye uchaguzi mkuu ujao kupitia muungano wa CORD, mwaka 2017.

Kiongozi wa WIPER Kalonzo Musyoka, amesema atamuunga mkono yeyote kati yao atakayeteuliwa na kwamba mpaka sasa wamejuana vyakutosha kuweza kupata mgombea mmoja.

Kwa upande wake, kinara wa ODM na waziri mkuu wa zamani, Raila Odinga, amesema kuwa anaamini kiongozi yeyote atakayeteuliwa na muungano wao, ataungwa mkono na wenzake, kama ambavyo yeye atamuunga mkono atakayeteuliwa.

Haya yanajiri wakati huu ambapo wachambuzi wa mambo wanaona kuwa itakuwa vigumu sana kwa viongozi hao kukubaliana licha ya kuwa wamekuwa kwenye muungano wao kwa muda mrefu, na kwamba nyakati kama hizi za uteuzi ndiko kunashuhudiwa baadhi ya miungano ikivunjika.

Hayo yakijiri waalimu katika shule nyingi za umma nchini Kenya wameendelea na mgomo wao kushinikiza Serikali kuwalipa nyongeza ya mshahara ya kati ya asilimia 50 na 60 kama ilivyoamriwa na mahakama ya juu juma moja lililopita, huku Serikali ikisisitiza kutokuwa na fedha hizo kwa wakati huu.

Waalimu sasa wanapanga kuishtaki katika mahakama ya kazi, tume ya kuajiri waalimu nchini Kenya, TSC, kwa madai ya kushindwa kutekeleza amri halali ya mahakama.

Shule nyingi kwenye maeneo mengi ya nchi zilishuhudia wanafunzi wakiwa nje ya madarasa wasijue cha kufanya baada ya waalimu kuendelea kutia ngumu kurejea kufundisha hadi pale watakapolipwa madai yao.

Katibu mkuu wa muungano wa walimu wa shule za Sekomdari nchini Kenya, Daniel Ndung'u anasisitiza kuwa walimu wao hawatorejea kazini hadi pale Serikali itakapotimiza madai yao.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.