Pata taarifa kuu
KENYA-MGOMO-ELIMU

Kenya: Mahakama yasimamisha agizo la serikali

Mahakama Kuu nchini Kenya imesimamisha agizo la serikali la kutaka shule zote ikiwa ni pamoja na zile za umma au za kibinafsi, zifungwe tangu Jumatatu wiki hii kutokana na mgomo wa waalimu.

Maandamano mbele ya jengo la Bunge, mjini Nairobi, Mei 14,i 2013, dhidi ya nyongeza ya mishahara kwa wabunge.
Maandamano mbele ya jengo la Bunge, mjini Nairobi, Mei 14,i 2013, dhidi ya nyongeza ya mishahara kwa wabunge. REUTERS/Thomas Mukoya
Matangazo ya kibiashara

Mahakama hiyo imetoa agizo hilo kufuatia kesi iliyowasilishwa na Chama cha Shule za Kibinafsi kupinga agizo la wizara ya elimu lililotolewa Ijumaa wiki iliyopita.

Serikali ilikuwa imeagiza wanafunzi wote kusalia nyumbani leo Jumatatu isipokuwa wale wanaojiandalia mitihani ya kitaifa.

Mahakama imesitisha agizo hilo upande wa shule za kibinafsi kwa siku tatu kusubiri kusikizwa kwa kesi hiyo.

Awali chama cha shule kilizitaka shule zote kukaidi agizo hilo, na kuendelea na masomo Jumatatu wiki hii. Baadhi ya shule zimeendelea kutoa visomo kama kawaida.

Wanafunzi wengi wa shule za umma wamelazimika kusalia nyumbani baada ya serikali kuagiza kufungwa kwa shule zote za umma na wale wanaosomea shule za mabweni wamelazimika kurudi nyumbani.

Hata hivyo mgomo wa walimu unaendelea kushuhudiwa nchini humo, huku ukiathiri mambo mengi ikiwa ni pamoja na kushuka kwa kiwango cha elimu kwa wanafunzi na wengi kwa sasa wamekua wakiranda randa hovyo mitaani.

Barua kutoka kwa wizara ya elimu iliagiza hivi karibuni shule zote za umma na za kibinafsi zifungwe na wanafunzi warudi nyumbani.

Wanafunzi wanaojiandaa kufanya mitihani ya kitaifa ya darasa la nane na kidato cha nne mwaka huu ndio watasalia shuleni pekee.

Chama cha walimu nchini Kenya KNUT kimefahamisha kuwa tayari kimepokea barua hiyo ya kufungwa kwa shule kutoka kwa serikali kuanzia jumatatu wiki hii.

Hivi karibuni muungano wa upinzani nchini Kenya CORD uliwaambia viongozi wao katika Bunge la kitaifa na lile la Senate kuandaa mswada wa kukosa imani na rais wa nchi hiyo Uhuru Kenyatta.

Wanasiasa wa upinzani walisema walichukua hatua hiyo kwa sababu rais Kenyatta ameshindwa kuiheshimu Katiba na kutii amri ya Mahakama ya kuitaka serikali kuwalipa walimu ili kumaliza mgomo unaoendelea.

Wiki iliyopita chama cha walimu wa shule za sekondari kilimtumia barua Spika wa bunge la kitaifa kuitisha kikao cha dharura kujadili suala la mgomo huu wa walimu.

Awali serikali ya Rais Uhuru Kenyatta ilisema haina pesa za kuwaongezea walimu mshahara, huku Wizara ya elimu ikisema mitihani ya kitaifa ya darasa la Nane na Kidato cha nne itaendelea kama ilivyopangwa, na uzinduzi wake ulifanyika Ijumaa wiki iliyopita.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.