Pata taarifa kuu
TANZANIA-UCHAGUZI-SIASA

ZEC yafuta matokeo ya uchaguzi Zanzibar

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi viziwani Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha ametangaza kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi visiwani humo akisema uchaguzi huo ulijaa kasoro nyingi.

Edward Lowasa mgombea wa Upinzani Tanzania.
Edward Lowasa mgombea wa Upinzani Tanzania. RFI-KISWAHILI
Matangazo ya kibiashara

Jecha Salim Jecha ametangaza hatua hiyo kupitia runinga ya serikali visiwani ZBC.

“ Uchaguzi haukuwa wa haki na kwamba kulikuwa na ukiukaji mkubwa wa sheria za uchaguzi, kwa mujibu wa taarifa ambayo baadaye imetumwa kwa vyombo vya habari ”, amesema Jecha Salim.

“ Baadhi ya makamishna wa Tume ya Uchaguzi, badala ya kutekeleza majukumu yao inavyotakiwa kikatiba "wamekuwa ni wawakilishi wa vyama vyao ", Jecha Salim Jecha ameongeza.

Jecha Salim Jecha amebaini kwamba kumegundulika kasoro nyingi katika uchaguzi huo miongoni mwa hizo ni kubainika kwa baadhi ya vituo hasa Pemba, ambavyo vimekuwa na kura nyingi kuliko daftari la wapiga kura wa kituo husika.

Hata hivyo Jecha Salim Jecha amesema kura hazikulindwa vilivyo hususan kisiwani Pemba ambako amesema kuwa baadhi ya mawakala wa baadhi ya vyama vya siasa katika kisiwa hicho walifukuzwa.

Mgombea wa chama cha upinzani cha CUF, Seif Sharif Hamad, alijitangaza kuwa mshindi siku moja baada ya uchaguzi kufanywa, hatua iliyokemewa na chama cha CCM.

Itafahamika kwamba mgombea wa CCM visiwani Zanzibar Ali Mohamed Shein amekuwa rais wa visiwa hivyo muhula unaomalizika.

Hayo yakijri mgombea urais kupitia muungano wa vyama vya upinzani UKAWA nchini Tanzania Edward Lowasa amesema hatambui matokeo ya urais yanayoendelea kutangazwa na tume ya uchaguzi nchini humo kutokana na kile anachosema kura zake zimeibiwa.

Akizungumza na wanahabari hapa jijini Dar es salaam, Lowasa ameitaka tume kusitisha mara moja kutangaza matokeo hayo na kutaka kura kuhesabiwa upya kutumia njia za kawaida bila kutumia teknolojia.

Lowasa amewataka wafuasi wake kuendelea kuwa watulivu wakati huu viongozi wa upinzani wanapoendelea na vikao kuhusu hatua zaidi watakazozichukua.

“ Nawaomba vijana wasalie katika hali ya utulivu na kuendelea kushikamana, tusilete vujo kwa sababu ukifanya hivyo tutawapa nafasi ya kuzungumza, tutawapa maelekezo zaidi ”, alisema Lowasa.

Nacho Chama cha mapinduzi kimekanusha madai hayo ya upinzani na kusema serikali haitakubali taifa hilo kuingia kwenye machafuko.

“ Ukawa wanaweza kulalamika usiku na mchana lakini hatuwezi kuruhusu nchi hii kuingia katika machafuko kwa sababu ya mtu mmoja ”, alisema mmoja wa viongozi wa CCM jijini Dar es salaam Jumatano jioni.

Hali hii imezua sintofahamu kati ya wafuasi wa Ukawa na CCM huku tume ya uchaguzi ikiendelea kutangaza matokeo ya urais.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Jaji Mstaafu Damian Lubuva amesema matangazo ya kura za urais yanatarajiwa kumalizika siku ya Alhamisi na baadaye mshindi kutangazwa na kukabidhiwa cheti.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.