DRC: Mapigano yaendelea kurindima karibu na Goma
Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wanajeshi wa serikali na waasi wa M23 wameendelea kupambana karibu na mji wa Goma, katika jimbo la Kivu Kaskazini, huku mjumbe wa amani kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta akitoa wito kwa makundi ya waasi kuweka silaha chini.
Imechapishwa:
Ripoti zinasema mapigano makali tangu hapo jana yamekuwa yakishuhudiwa katika êneo la Kibumba, karibu Kilomita 20 kutoka mji wa Goma.
Aidha, ripoti zingine za kiusalama zimesema waasi wa M 23 wameonekana katika mbunga ya taifa ya Virunga.
Wakati mapigano hayo yakiendelea, na kuwapa wasiwasi wakaazi wa Kivu Kaskazini hasa mjini Goma, mjumbe kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta amemaliza ziara yake ya siku mbili jijini Kinshasa, kuelekea mazungumzo ya amani wiki ijayo jijini Nairobi.
Wakazi wa Mashariki wma DRC, wanasubiri kuona iwapo juhudi hizi za kidiplomazia zitasaidia na kuzaa matunda ya kuleta utulivu Mashariki mwa nchi yao.