Pata taarifa kuu

Guinea: Kesi ya Dadis Camara kuanza kusikilizwa tena Jumatatu baada ya kuondolewa gerezani

Kesi ya kihistoria ya mauaji ya Septemba 2009 nchini Guinea itaanza kusikilizwa Jumatatu, siku tisa baada ya operesheni ya kundi la watu waliojihami kwa silaha kuwaondoa jela washtakiwa wanne, akiwemo kiongozi wa zamani Moussa Dadis Camara, amesema mmoja wa wwsemaji wa kundi linaloandaa kesi hiyo.

Moussa Dadis Camara alihojiwa na majaji wawili wa uchunguzi na mwendesha mashtaka wa Guinea huko Ouagadougou kwa zaidi ya saa mbili, Jumatano Julai 7, 2017.
Moussa Dadis Camara alihojiwa na majaji wawili wa uchunguzi na mwendesha mashtaka wa Guinea huko Ouagadougou kwa zaidi ya saa mbili, Jumatano Julai 7, 2017. © AFP PHOTO / AHMED OUOBA
Matangazo ya kibiashara

Washtakiwa watatu, akiwemo Moussa Dadis Camara, walikamatwa tena siku hiyo hiyo, Novemba 4. Mmoja wao, Kanali Claude Pivi, bado yuko mafichoni na hatakuwapo Jumatatu isipokuwa aweze kukamatwa na kuwekwa jela.

Shambulio la Novemba 4, ambalo lilisababisha vifo vya watu tisa kwa mujibu wa mamlaka, lilizua hofu ya kuendelea kwa kesi hiyo iliyofunguliwa Septemba 28, 2022 baada ya miaka mingi waathiriwa wakisubiri. Mamlaka imehakikisha kwamba kesi hiyo itaendelea.

Siku ya Jumamosi jioni Abdoulaye Djibril Diallo, msemaji wa kundi linaloandaa kesi hiyo, alibaini kwenye runinga ya serikali kwamba kesi hiyo itaanza kusikilizwa siku ya Jumatatu.

Kesi hiyo ilisitishwa kwa wiki tatu, kwanza kwa ombi la mwendesha mashtaka ambaye aliomba muda wa kujiandaa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa kwa mashahidi, kisha kutokana na mgomo wa mawakili usiohusiana na kesi hiyo au matukio ya tarehe 4 Novemba.

Moussa Dadis Camara na maafisa wengine kumi wa zamani wanashitakiwa kwa mauaji, vitendo vya utesaji, ubakaji na utekaji nyara mwingine uliofanywa mnamo Septemba 28, 2009 na siku zilizofuata na vikosi vya usalama katika uwanja wa michezo katika vitongoji vya Conakry, ambapo makumi ya maelfu ya wafuasi wa upinzani walikusanyika ndani na karibu na eneo hilo.

Takriban watu 156 waliuawa na mamia kujeruhiwa, na wanawake wasiopungua 109 kubakwa, kulingana na ripoti ya tume ya uchunguzi iliyopewa mamlaka na Umoja wa Mataifa.

Majaji na mawakili wamewahoji washtakiwa na mashirika ya kiraia katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Baada ya jaribio la kutoroka Novemba 4, utawala wa kijeshi uliwafukuza kazi karibu maafisa sitini, askari na maafisa katika idara ya usalama na katika jela walikokuwa wanazuiliwa washtakiwa. Afisa katika Wizara ya Sheria ameliambia shirika la habari la AFP kwa sharti la kutotajwa jina kwamba karibu watu sitini wamekamatwa.

Katika siku za hivi majuzi, Waziri wa Sheria Alphonse Charles Wright alizungumza wazi juu ya njama ndani ya idara za usalama.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeelezea wasiwasi wake kuhusu usalama wa waathiriwa wa mauaji hayo katika taarifa.

Chama cha wanasheria kimeripoti katika taarifa "makosa na unyanyasaji" uliofanywa na vikosi vya usalama wakati wa kumsaka Claude Pivi. Chama hiki kiliripoti vitisho vilivyotolewa dhidi ya baadhi ya mawakili wa watuhumiwa wa mauaji hayo, na kimeiomba Serikali kuwalinda.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.