Pata taarifa kuu
BURUNDI-SIASA

Chama cha Cndd-Fdd chamteua Nkurunziza

Chama tawala cha Cndd-Fdd nchini Burundi kimemteua Jumamosi Aprili 25 rais Pierre Nkurunziza kugombea katika uchaguzi ujao wa urais unaopangwa kufanyika Juni 26.

Chama tawala Burundi cha Cndd-Fdd chafanya kongamano kuu Jumamosi Aprili 25 mwaka 2015 la kumteua rais Pierre Nkurunziza ( katikati )  kugombea katika uchaguzi wa urais. Raia wajawa na hofu ya kutokea machafuko.
Chama tawala Burundi cha Cndd-Fdd chafanya kongamano kuu Jumamosi Aprili 25 mwaka 2015 la kumteua rais Pierre Nkurunziza ( katikati ) kugombea katika uchaguzi wa urais. Raia wajawa na hofu ya kutokea machafuko. Photo : RFI / Sonia Rolley
Matangazo ya kibiashara

Hata hivyo rais Pierre Nkurunziza alionekana tangu awali kuwa ndiye angeligombea kwenye nafasi hiyo, viongozi mbalimbali katika mikutano yao wamekua wakitaja kuwa mgombea katika uchaguzi wa urais kwa tiketi ya chama tawala cha Cndd-Fdd ni ule ule, hapa wakimaanisha Pierre Nkurunziza.

Wakati huohuo raia mjini Bujumbura wamejawa na hofu kutokana na hali hiyo. Tangu chama cha Cndd-Fdd kutangaza mwanzoni mwa wiki hii kuwa kitafanya kongamano Jumamosi mwishoni mwa juma hili, wakaazi wengi wa mji wa Bujumbura wamekua wakinunua chakula kwa wingi na kuweka akiba, wakihofia kutokea kwa machafuko, baada ya kutangazwa jina la Pierre Nkurunziza kama mgombea wa chama tawala cha Cndd-Fdd katika uchaguzi ujao wa urais, unaopangwa kufanyika Juni 26 mwaka 2015.

Hata hivyo idadi ya raia wa Burundi wanaoendelea kuitoroka nchi na kukimbilia katika mataifa jirani imeendelea kuongezeka. Raia wengi mikoni wameitoroka nchi hususan katika mikoa ya kazkazini, magharibi na kusini mwa nchi. Wengi wanabaini kwamba wanahofia usalam wao kufuatia kauli zinazotolewa na vijana wa chama tawala , Imbonerakure, ambao wamekua wakiandaman katika mikoa mbalimbali wakisema kuwa anayepinga muhula watatu wa rais Nkurunziza watakiona cha mtima kuni, kwa mujibu wa raia hao wanaoitoroka nchi.

Awali, baadhi ya viongozi serikali nchini Burundi walisikika wakisema kwamba watu hao wanaoitoroka nchi, wanakimbia amani, huku wengine wakibaini kwamba wengi wanaokimbia, wanahusika na makosa mbalimbali.

Chama cha Cndd-Fdd kinatazamia kumteua Nkurunziza kama mgombea wake katika uchaguzi wa urais wakati vyama vya upinzani na mashirika ya kiraia, bila kusahau baadhi ya wafuasi wa chama cha Cndd-Fdd wakiendelea kupinga rais Nkurunziza kugombea muhula watatu.

Chama tawala Burundi cha Cndd-Fdd chafanya kongamano kuu Jumamosi Aprili 25 mwaka 2015 la kumteua rais Pierre Nkurunziza kugombea katika uchaguzi wa urais.
Chama tawala Burundi cha Cndd-Fdd chafanya kongamano kuu Jumamosi Aprili 25 mwaka 2015 la kumteua rais Pierre Nkurunziza kugombea katika uchaguzi wa urais. RFI/Karim Nkeshimana

Hivi karibuni vyama vitano vya upinzani pamoja na kundi la wafuasi wa chama cha Cndd-Fdd vilitolea wito wafuasi wao kuingia mitaani kwa kupinga nia ya rais Nkurunziza ya kugombea muhula watatu.

Alhamisi wiki hii, vyama vya kiraia vilitolea wito raia kuingia mitaani Jumapili asubuhi mwishoni mwa juma hili iwapo chama cha Cndd-Fdd kitatangaza Jumamosi Aprili 25 jina la Pierre Nkurunziza kama mgombea wa chama hicho katika uchaguzi wa urais wa Juni 26.

Viongozi mbalimbali kutoka Marekani Ulaya, taasisi za Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Afrika Mashariki, shirika la marais wa zamani wa Afrika pamoja Kanisa katoliki nchini Burundi walimsihi rais Nkurunziza kutogombea muhula watatu, ambao ni kinyume na Katiba pamoja na Mkataba wa amani wa Arusha, kwa hofu ya kuitumbukiza nchi ya Burundi katika machafu kama yale yaliyoikumba nchi hiyo kwa kipindi cha mwongo mmoja tangu mwaka 1993, lakini Pierre Nkurunziza ameendelea kupuuzia nasaha hiyo, na amekua akionyesha nia yake ya kugombea muhula watatu bila kujali chochote.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.