Pata taarifa kuu
BURUNDI-USHIRIKIANO-USALAMA-SIASA

Ufaransa yasitisha ushirikiano wake wa kiusalama na Bujumbura

Ufaransa imesitisha ushirikiano wake wa kiusalama na Burundi katika nyanja ya polisi na ulinzi, chanzo cha kidiplomasia cha Ufaransa mjini Bujumbura kimebaini. Uamzi huo unakuja wakati Burundi inakabiliwa kwa kipindi cha mwezi mmoja na wimbi la maandamano ya raia dhidi ya muhula wa tatu wa rais Pierre Nkurunziza.

Waandamanaji wanaopinga muhula wa tatu wa rais Pierre Nkurunziza katika wilaya ya Cibitoke, kaskazini mwa Bujumbura, Mei 22..
Waandamanaji wanaopinga muhula wa tatu wa rais Pierre Nkurunziza katika wilaya ya Cibitoke, kaskazini mwa Bujumbura, Mei 22.. AFP PHOTO/ CARL DE SOUZA
Matangazo ya kibiashara

Wakati huo huo ikiwa ni mara ya kwanza tangu Burundi ikumbwe na maandamano ya raia wakipinga muhula wa tatu wa rais Pierre Nkurunziza, serikali ya Bujumbura imeionya usiku wa Jumatatu Mei 25 kuamkia Jumanne 26 jumuiya ya kimataifa kutoingilia masuala ya katiba ya nchi hiyo. Msemaji wa serikali ya Burundi, Philippe Nzobonariba amesema akisisitiza kuhusu haja ya kuheshimu taasisi za Burundi.

" Serikali ya Burundi inapenda kusisitiza haja ya kuheshimu taasisi husika za Burundi. Katika suala hili, Serikali ya Burundi haitozungumza wala kujadili masuala ambayo yanalenga kuzorotesha taasisi zake. Huu ni mstari mwekundu ambao ni muongozo kwa wale ambao wanataka kushirikiana na serikali. Rais Nkurunziza ameelezea kuwa kama atachaguliwa na wananchi kwa kufuatisha Katiba, itakuwa muhula wake wa mwisho ", amesema Nzobonariba.

Hayo yanajiri wakati kunatazamiwa kufanyika mkutano mpya wa kikanda wa marais kutoka nchi za Afrika mashariki, ambazo ni Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda na Burundi, mkutano ambao utafanyika Jumapili mwishoni mwa juma hili jijini Dar es Salaam, nchini Tanzania. Mkutano huo unalenga kutafutia ufumbuzi na kuchukua uamzi mara moja kuhusu muhula wa tatu wa rais Nkurunziza na kukomesha visa vya unyanyasaji vinavyoendelea kushuhudiwa nchini Burundi.

Wafadhili wa Burundi wanaendelea kuchukua uamzi wa kusitisha misaada kwa taifa hilo dogo la Afrika ya Kati. Baada ya Ubelgiji, Uholanzi, Uswisi na Marekani, Ufaransa imechukua leo Jumanne uamzi wa kusitisha ushirikiano wake wa kiusalama na serikali ya Bujumbura.

Wakati huo huo maandamano yameendelea Jumanne wiki hii katika mji wa Bujumbura. Wilaya ya Buyenzi ambayo imekua haijakumbwa na maandamano hayo tangu kushindwa kwa jaribio la mapinduzi siku 13 zilizopita, leo Jumanne shughuli zimekwama wilayani humo kutokana na maandamano.

Umoja wa Ulaya umewaondoa wafanyakazi wake nchini Burundi. Uamzi huo wa Umoja wa Ulaya unakuja baada ya Marekani, na mashirika ya kimataifa kuwaondoa wafanyakazi wao nchini humo kufuatia hali ya usalama ambayo imeendelea kudorora.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.