Pata taarifa kuu
USALAMA-AMANI

Somalia: Hali yarejea kuwa shwari, washambuliaji wote wauawa

Shambulio lililotekelezwa na wapiganaji wa kundi la Al Shabab dhidi ya Hoteli moja katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu siku ya Alhamisi jioni limemalizika, polisi imetangaza leo Ijumaa, na kuongeza kuwa "washambuliaji wote wameuawa." Hakuna tathmini ya shambulio hilo iliyotolewa mara moja.

Hoteli hiyo ilikuwa ikilengwa mara kadhaa tangu mwaka 2015 na Al Shabab. Wakati wa shambulio la hivi karibuni, mnamo mwezi Desemba 2019, watu watano, raia watatu na maafisa wawili wa vikosi vya usalama, waliuawa.
Hoteli hiyo ilikuwa ikilengwa mara kadhaa tangu mwaka 2015 na Al Shabab. Wakati wa shambulio la hivi karibuni, mnamo mwezi Desemba 2019, watu watano, raia watatu na maafisa wawili wa vikosi vya usalama, waliuawa. REUTERS/Feisal Omar
Matangazo ya kibiashara

"Magaidi wote wenye silaha wameuawa na hali imerejea kuwa ya kawaida, vikosi vya usalama vinafanya ukaguzi na uchunguzi," Abdirahim Yusuf, afisa wa polisi, ameliambia shirika la habari la AFP. Alikuwa akizungumza karibu saa 13 baada ya Al Shabab kuzindua shambulio hilo dhidi ya Hoteli ya SYL, iliyoko karibu na eneo lenye ulinzi mkali la Villa Somalia, jumba ambalo kupatikana ikulu ya rais wa Somalia na ofisi za Waziri Mkuu.

Shambulio hilo linalodaiwa na kundi la Kiislamu lenye mafungamano na Al-Qaeda, lilianza siku ya Alhamisi mwendo wa 3:45 usiku (saa za Somalia) wakati watu waliokuwa na silaha walipovamia hoteli ya SYL na kuanza kufyatua risasi. "Watu kadhaa waliokuwa na silaha waliingia ndani ya jengo hilo kwa nguvu baada ya kuharibu ukuta jengo hilo kwa vilipuzi," afisa wa usalama Ahmed Dahir ameliambia shirika la habari la AFP muda mfupi baada ya kuanza kwa mashambulizi.

Walioshuhudia wamesema walisikia washambuliaji wakipiga risasi kiholela. Milio ya risasi na milipuko ya hapa na pale ilisikika kwa saa kadhaa. "Sijui kama kuna waathiriwa wowote, lakini kulikuwa na watu wengi ndani ya Hoteli hiyo wakati shambulio hilo lilipoanza," amesema Hassan Nur, ambaye aliweza kutoroka kwa kupanda ukuta.

Hoteli hiyo ilikuwa ikilengwa mara kadhaa tangu mwaka 2015 na Al Shabab. Wakati wa shambulio la hivi karibuni, mnamo mwezi Desemba 2019, watu watano, raia watatu na maafisa wawili wa vikosi vya usalama, waliuawa. Al Shabab imekuwa ikipigana na serikali ya shirikisho ya Somalia, inayoungwa mkono na jumuiya ya kimataifa, kwa zaidi ya miaka 16.

Waasi hawa wanaohusishwa na Al-Qaeda walidhibiti mji mkuu hadi 2011, walipofukuzwa na askari wa Umoja wa Afrika. Lakini Al Shabab bado imeanzishwa katika maeneo makubwa ya vijijini katikati na kusini mwa nchi, ambapo mara kwa mara hufanya mashambulizi dhidi ya malengo ya usalama, kisiasa na kiraia. Wamechukuliwa kuwa kundi la kigaidi na Washington tangu 2008.

Serikali ya Rais Hassan Cheikh Mohamoud ilianzisha mashambulizi makubwa mwezi Agosti 2023, ikisaidiwa na jeshi la Marekani na kikosi cha Umoja wa Afrika kilichopo nchini humo (Atmis), ambayo, baada ya kuweza kudhibiti upya maeneo ya katikati mwa Somalia, kwa sasa operesheni hiyo imesitishwa.

Siku ya Alhamisi, rais wa Somalia alifanya "mkutano wa kimkakati" na maafisa wa ulinzi kupanga udhibiti mpya wa maeneo waliyopoteza, shirika la habari la Sonna limeripoti. "Rais alisifu juhudi shupavu za vikosi vya Somalia na kuangazia dhamira isiyoyumba ya serikali ya kutokomeza ugaidi," kulingana na Sonna.

Mnamo Januari, Al Shabab walichukua mateka kadhaa baada ya kukamata helikopta ya Umoja wa Mataifa ambayo ililazimika kutua kwa dharura katikati mwa nchi.

Mnamo Mei 26, Al Shabab ilishambulia kambi iliyokuwa na wanajeshi wa Uganda wa kikosi cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (Atmis) kusini mwa nchi hiyo, na kuua takriban wanajeshi 54. Mnamo Oktoba 29, 2022, mabomu mawili yaliyotegwa katika gari yalilipuka huko Mogadishu, na kuua watu 121 na kujeruhi 333, shambulio baya zaidi kuwahi kutokea katika miaka mitano nchini Somalia pia iliyoathiriwa na ukame wa kihistoria.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.