Pata taarifa kuu

Pamoja na Japan na Korea Kusini, Joe Biden atuma ujumbe wa umoja kwa China

Joe Biden siku ya Ijumaa aliwapokea viongozi wa Japan na Korea Kusini huko Camp David, karibu na Washington, kwa mkutano aliouita wa "kihistoria" na ambaye alituma ujumbe mzito wa umoja kwa China.

Rais wa Marekani Joe Biden akiwa na Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida na rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol huko Camp David mnamo Agosti 18, 2023.
Rais wa Marekani Joe Biden akiwa na Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida na rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol huko Camp David mnamo Agosti 18, 2023. AP - Alex Brandon
Matangazo ya kibiashara

Akiandamana na Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida na rais wa Korea Kusini Yoon Suk-yeol kwa mkutano na waandishi wa habari, rais wa Marekani alitangaza kwamba nchi hizo tatu zitashauriana kwa utaratibu na "haraka" katika siku zijazo dhidi ya "vitisho" vinavyowalenga.

"Tunakusudia kupeana taarifa zetu, kuratibu jumbe zetu na majibu yetu," walihakikishia viongozi hao watatu katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyochapishwa kuhusu suala hilo. Hata hivyo Joe Biden alisifu "ujasiri wa kisiasa" wa wageni wake, ambao wamefanya kazi kuleta nchi zao mbili karibu pamoja licha ya kipindi kilichopita cha maumivu ya ukoloni wa Korea Kusini na Japan.

“Hatuzungumzii siku moja, wiki moja au mwezi mmoja. Ni miongo” ya ushirikiano, alibainisha rais wa Marekani kuhusu mazungumzo haya yaliyoimarishwa, ambayo tayari yamekosolewa vikali na Beijing. Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa siku ya Ijumaa, Marekani, Japan na Korea Kusini pia zililaani "tabia hatari na ya uchokozi" ya China na "madai haramu ya baharini" kutoka China katika masuala ya baharini, katika taarifa ya pamoja iliyotolewa siku ya Ijumaa, huku kukiwa na mvutano kati ya Beijing na Ufilipino kuhusu suala la usalama wa baharini.

Mazoezi ya pamoja ya kijeshi na njia ya mawasiliano ya dharura

Mkutano huo ulifanyika Camp David, chaguo ambalo sio kwa bahati mbaya, anabainisha mwandishi wetu wa New York, Loubna Anaki. Ni katika Camp David ambapo mijadala mingi ya hali ya juu imefanyika. Hapa ndipo palipotiwa saini mkataba mashuhuri wa Camp David Accords, mikataba ya amani kati ya Misri na Israel. Rais Roosevelt alimpokea Winston Churchill Camp David wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Kwa hivyo sio bahati mbaya kwamba Joe Biden kuchagua makazi haya kwa minajili ya mkutano huu. Itafahamika kuwa hii ni mara ya kwanza tangu 2015 kwa viongozi wa kigeni kupokelewa Camp David. Hii inaashiria umuhimu wa mkutano huu na wadau wake.

  "Tunapinga vikali jaribio lolote la upande mmoja la kubadilisha hali iliyopo katika eneo la Indo-Pasifiki," walisema viongozi wa nchi hizo tatu katika taarifa hii ya pamoja, yaliyopewa jina la "The Spirit of Camp David". Wanaongeza: "Tunathibitisha tena umuhimu wa amani na utulivu katika Mlango-Bahari wa Taiwan". Pia walitoa wito kwa Korea Kaskazini "kuachana na mpango wake wa nyuklia na makombora ya balestiki".

Nchi hizo tatu zitaanzisha mpango wa mazoezi ya pamoja ya kijeshi kwa miaka kadhaa. Lakini kulingana na mshauri mkuu wa usalama wa Ikulu ya White House, Jake Sullivan, ushirikiano huu ulioimarishwa "sio NATO kwa Pasifiki", ambayo ni muungano wa ulinzi wa pande zote. Marekani, Japan na Korea Kusini pia hujitolea kufanya mkutano huo wa viongozi wao kila mwaka.

Pia wataweka njia ya mawasiliano ya dharura katika kiwango cha juu zaidi, aina ya simu nyekundu katika eneo ambalo likochini ya tishio la mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini na linahofia kuvamiwa kwa Taiwan na China. Akiwa Camp David, Joe Biden hata hivyo alionyesha kwamba bado ana nia ya kukutana na mwenzake wa China, Xi Jinping, mwezi Novemba nchini Marekani kwa ajili ya mkutano wa kilele wa Asia-Pacific (Apec).

(Pamoja na AFP)

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.