Pata taarifa kuu

Bangladeshi: Kampuni za kutengeneza nguo zafunga kufuatia maandamano ya kudai mishahara

Kampuni za kutengeneza nguo nchini Bangladeshi, zimelazimika kufunga viwanda 150 "kwa muda usiojulikana" Jumamosi, Novemba 11, wakati sekta ya nguo inakabiliwa na ongezeko kubwa la madai ya mishahara, ambayo yamesababisha polisi kuwafungulia mashitaka wafanyakazi 11,000 kwa vurugu, mamlaka imetangaza.

Bangladesh Industrie Textile manifestations
Maandamano ya wafanyakazi wa tasnia ya nguo huko Dhaka (Bangladesh), Novemba 10, 2023. AFP - MUNIR UZ ZAMAN
Matangazo ya kibiashara

Bangladeshi, nchi maskini huko Asia Kusini, imetikiswa tangu Oktoba 2023 na maandamano yenye vurugu ya wafanyakazi wa nguo wanaodai mishahara bora. Maandamano hayo yamesababisha vifo vya wafanyakazi wasiopungua watatu na zaidi ya viwanda 70 viliporwa au kuharibiwa, kulingana na polisi. Kamati ya kima cha chini cha mishahara ya sekta ya nguo wiki hii ilipendekeza nyongeza ya 56.25% katika mshahara wa kimsingi wa kila mwezi wa wafanyakazi milioni nne wa sekta hiyo, na kufikisha hadi taka 12,500 (sawa na euro 104), kiasi ambacho kilichukuliwa kuwa "udhalili" na kukataliwa mara moja na vyama vya wafanyakazi.

Makabiliano na polisi

Siku ya Alhamisi, Novemba 9, wafanyakazi wapatao 15,000 walipambana na polisi kwenye barabara kuu na kupora Tusuka, kiwanda kikubwa, na viwanda kadhaa vingine. "Polisi wamefungua mashtaka dhidi ya watu 11,000 wasiojulikana kufuatia shambulio kwenye kiwanda cha nguo cha Tusuka," inspekta wa polisi Mosharraf Hossain ameliambia shirika la habari la AFP. Vikosi vya usalama vya Bangladeshi mara nyingi huwashtaki maelfu ya watu - bila kutaja majina yao - kufuatia maandamano makubwa na vurugu za kisiasa, mbinu ambayo wakosoaji wanasema ni njia ya kuwakandamiza wapinzani.

Maafisa wa polisi wameliambia shirika la habari la AFP kuwa viwanda 150 vimefungwa katika miji mikuu ya viwanda ya Ashulia na Gazipur, yote miwili inayopatikana kaskazini mwa mji mkuu Dhaka, huku watengenezaji wakihofia migomo zaidi ya wiki ya kazi nchini Bangladesh ambayo inaanza Jumamosi.

Changamoto kubwa kwa serikali

Maandamano kuhusu madai ya mishahara yanaleta changamoto kubwa kwa Waziri Mkuu Sheikh Hasina, ambaye ameitawala nchi hiyo kwa mkono wa chuma tangu mwaka 2009. Upinzani unaoibuka tena unapinga mamlaka yake, huku akikabiliwa na uchaguzi uliopangwa kabla ya mwisho wa mwezi wa Januari 2024. Viwanda 3,500 vya kutengeneza nguo nchini Bangladeshi vinawakilisha takriban 85% ya dola bilioni 55 katika mauzo ya nje ya kila mwaka, na kusambaza bidhaa nyingi kuu za kimataifa, zikiwemo za Levi's, Zara na H&M. Lakini mazingira ya kazi kwa wengi wa wafanyakazi milioni nne wa sekta hiyo, wengi wao wakiwa wanawake, ni mabaya.

(Pamoja na AFP)

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.